IQNA

Imam Khamenei: Maendeleo makubwa ya Iran yamefelisha njama za mabeberu

0:04 - June 04, 2012
Habari ID: 2339788
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba, maendeleo ya taifa la Iran katika sekta ya sayansi na teknoloji pamoja na kuzishinda changamoto za kisiasa, kijeshi, kiusalama na kiuchumi katika miaka 33 iliyopita, ni mambo ambayo yamefelisha njama za mabeberu wa dunia za kutaka kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo Jumapili, Juni 3, 2012, amehutubia umati mkubwa wa muhibu na wapenzi wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) katika Haram tukufu na Mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema katika hotuba yake kuwa, Imam (Mwenyezi Mungu amrehemu) ni baba wa taifa la Iran na ni dhihirisho la upole, nguvu na kusimama imara.
Vile vile ameashiria jitihada zenye muono wa mbali za Imam katika kuhuisha roho ya heshima ya taifa na kuimarisha muundo wa ndani wa taifa la Iran na kuongeza kuwa, historia iliyojengwa na Iran kwa kutegemea mambo hayo imetoa somo na kigezo cha Iran ya Kiislamu na maendeleo, nje ya mipaka ya eneo la ushawishi wa mabeberu wa dunia, kwa ajili ya mataifa mengine na kuwatia kiwewe waistikbari duniani.
Amesema njia hii inayong'aa itaendelea hadi kufikia kwenye vilele vya juu vya maendeleo na kuwakatisha tamaa kikamilifu maadui na kwamba ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kuwa, mustakbali wa mataifa ya Waislamu na taifa la Iran unang'ara na kumeremeta.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika leo asubuhi kwa hamasa na shauku kubwa kwa ajili ya kukumbuka mwaka wa 23 wa kufariki dunia Kiongozi kabiri wa Mapinduzi ya Kiislamu; Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia idi yenye baraka ya kukumbuka siku ya kuzaliwa baba wa Umma, Amirul Muuminin Ali bin Abu Talib (Alayhis Salaam) na kutangazwa siku ya mwezi 13 Rajab kuwa siku ya baba nchini Iran na kusisitiza kuwa: Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini) kwa hakika alikuwa baba mzuri sana wa taifa hili kwani kwa upande mmoja alikuwa ni dhihirisho la upole na huruma ya baba kwa wanawe na katika upande wa pili alikuwa ni dhihirisho la nguvu na kusimama imara.
Aidha amemtaja Imam Khomeini (quddisa sirruh) kuwa ni baba wa harakati ya Kiislamu inayoshuhudiwa leo hii katika ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa, moja ya njia kuu za sira na mwenendo wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu awe radhi naye) ni kupuliza roho ya heshima ya taifa la Iran na kulihuisha na kulipa uhai mpya taifa hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja mjadala kuhusu harakati kubwa ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) ya kupuliza roho ya heshima kwa taifa na kwa nchi ya Iran kuwa si mjadala wa kinadharia bali ni maudhui iliyosimama juu ya matukio ya kweli katika jamii.
Aidha amebainisha mantiki ya Qur'ani kuhusiana na heshima na kufafanua akisema: Katika mantiki ya Qur'ani, heshima ya kweli na kamili ni ya Mwenyezi Mungu na ni ya kila mtu ambaye yumo katika kambi ya Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa mantiki ya Qur'ani, inabidi heshima itafutwe na iombwe kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa: Wakati mtu au jamii inapopata heshima ya kweli, heshima hiyo huwa mithili ya kinga imara inayofelisha juhudi zote za adui za kutaka kujipenyeza au kuizingira na kuiangamiza jamii hiyo.
Amesisitiza kuwa, kadiri heshima hiyo inapoenea na kukita vilivyo kwenye matabaka ya kila mtu na ya jamii yote kwa pamoja, ndivyo jamii na watu hao wanavyozidi kuwa na kinga imara isiyoweza kupenyeka na hatimaye mtu na jamii hufiikia katika hatua ambayo inaiwezesha jamii na mtu huyo kuwa salama mbele ya adui mkubwa wa mwanadamu yaani shetani.
Kiongozi Muadhamu wa Mpainduzi ya Kiislamu, amemtaja Imam Khomeini (quddisa sirruh) kuwa ni mfano wa wazi wa heshima ya namna hiyo na kuongeza kuwa: Katika kipindi chote cha uhai wake, Imam (Mwenyezi Mungu amrehemu) alikuwa ni misdaki na dhihirisho la wazi la kutawakali kwa Mwenyezi Mungu Azizi na Mrehemevu, iwe ni katika upande wa elimu na usomeshaji, au katika kipindi kigumu cha mapambano au katika wakati wa kuongoza na kuendesha nchi na taifa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kwamba: Ni kwa sababu hiyo ndio maana kazi kubwa ambazo watu wote walikuwa wanasisitiza kuwa haziwezekani ziliwezekana kwa kujitokeza Imam na vizuizi vyote ambavyo vilikuwa ni muhali kuvunjwa na kuondolewa, viliweza kuondolewa kwa kuja Imam.
Amesisitiza pia kuwa, sambamba na kwamba Imam wetu mtukufu alikuwa ni dhihirisho la heshima ya nafsi na umaanawi, aliweza pia kupuliza roho ya heshima kwa taifa la Iran na kulipa uhai mpya taifa hilo.
Amesisitiza akisema: Kutokana na taifa la Iran kupata hisia za heshima ilizojifunza kutoka katika mafundisho ya Mapinduzi ya Kiislamu na kutoka kwa Imam, limeweza kugundua uwezo wake na sote tunashuhudia kwa macho yetu jinsi ahadi nyingi mno za Mwenyezi Mungu zinavyotimia ikiwa ni pamoja na ushindi wa wanyonge mbele ya mabeberu na waistikbari.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia tarikhi na historia iliyojaa misukosuko ya Iran na kukumbusha kuwa: Katika historia yetu ndefu sisi Wairani, tumepitia nyakati tofauti, na tumeshuhudia nyakati za heshima na udhalilifu ambapo kipindi cha miaka 200 iliyomalizikia kwenye Mapinduzi (ya Kiislamu), kilikuwa ni kipindi kigumu, kipindi kilichojaa kiza na udhalilifu (kwetu).
Amekutaja kutengwa katika eneo na duniani, kubakishwa nyuma vibaya katika masuala ya kiuchumi, kubakishwa nyuma kiuhakiri katika masuala ya sayansi na teknolojia na kuwa duni na dhaifu kupindukia tawala za watawala wa kipindi hicho cha karne mbili nchini Iran mbele ya wakoloni na mbele ya mabeberu wa kigeni kuwa ni miongoni mwa ushahidi wa wazi wa udhalilifu uliolikumba taifa la Iran katika kipindi cha tawala za wafalme wa Kikajari na Kipahlavi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia mikataba ya kujidunisha na kulidhalilisha taifa iliyopelekea Iran kupoteza makumi ya miji yake azizi na kuongeza kuwa, katika kipindi hicho kilichojaa uduni na udhalili, wageni kutoka nje waliweka vibaraka wao kuitawala Iran katika kalibu ya utawala wa Kipahlavi na kuigeuza Iran kuwa medani ya kuendeshea vita vya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
Vile vile ametoa ufafanuzi kuhusu misdaki na ushahidi wa wazi wa vitendo vya kujidunisha na kujidhalilisha vya watawala wa Iran katika kipindi cha karne mbili za kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya ubeberu na uistikbari wa wageni na kuongeza kuwa: Tab'an katika kipindi hicho pia kulikuwa na vitu vilivyojipambanua na masuala mengine ya wakati huo kama vile Amir Kabir, fatwa na Ayatullah Shirazi na kadhia ya Tumbaku, kushiriki maulamaa wa kidini katika kadhia ya kipindi cha utawala wa katiba na mwamko wa kuyafanya mafuta ya Iran kuwa mali ya taifa, lakini mambo hayo imma yalikuwa ya muda mfupi au yalifeli na kushindwa kikamilifu na hivyo taifa hili kubwa lililojenga historia (katika miongo hii mitatu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu) likaendelea kuwa dhaifu na kudhalilishwa.
Ayatullah Udhma Khamenei, ameyataja Mapinduzi kabiri na adhimu ya Kiislamu ya nchini Iran kuwa yalitia kikomo mwenyendo wa kudhalilishwa taifa la Iran na kufungua ukurasa mpya wa kupata heshima taifa hili na kusisitiza kuwa: Baada ya ushindi wa Mapinduzi (ya Kiislamu), ukurasa uligeuka kikamilifu na kutokana na Imam Khomeini kutilia mkazo mno suala la kuhuisha na kufufua roho ya heshima ya taifa aliweza (kubadilisha fikra potofu ya kujiona duni iliyokuwa imepandikizwa katika taifa hili na) mahala pake kuweka utamaduni wa "sisi tunaweza" ndani kabisa ya moyo wa taifa hili la waumini.
Pia ametoa ushahidi kutoka katika Qur'ani Tukufu na kusema kwamba, kitendo cha kuwa na imani chenyewe kinaleta heshima akiongeza kuwa: Imam mtukufu na kiongozi huyo mwenye busara wa taifa, alipata njia za kufufua misukumo na hima, akafanikiwa kuliingiza katika medani taifa la waumini na hatua ya wananchi ya kujitokeza vilivyo katika medani ikafanikisha kivitendo sunna tukufu ya Mwenyezi Mungu ya kuandaa mazingira ya kuminikiwa taifa hili na rehema zisizo na kifani za Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia juu ya muundo wa ndani wa taifa la Iran na kwamba muundo huo wa ndani ulikuwa ni nukta kuu iliyokuwemo kwenye fasihi ya Imam Khomeini na kuongeza kuwa: Katika kuhuisha roho ya heshima ya taifa, Imam hakutegemea mambo ya fakhari na majivuno bali alilitia nguvu jengo hili kwa kuliimarisha taifa kwa ndani na jambo hilo limepelekea roho ya heshima ya taifa na ustawi iendelee kushuhudiwa hadi hivi sasa ndani ya nchi hii kubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, kuweza kukabiliana na vitu vinavyopelekea kuzorota na kukukwama harakati za taifa ni sharti la kuendelea njia ya ustawi na heshima ya taifa na kuongeza kuwa: Baadhi ya mambo yanayoweza kukwamisha maendeleo katika kipindi hiki ni sisi wenyewe na baadhi yake ni mambo ya kutwishwa na maadui na kama hatutaki tukumbwe tena na mazingira ya jahanamu yaliyokuwepo kabla ya Mapinduzi (ya Kiislamu), basi hatuna njia nyingine isipokuwa kupambana vilivyo na kwa busara ya hali ya juu na mambo yote hayo (yanayoweza kukwamisha harakati ya taifa).
Vile vile ameashiria sababu za muongo huu wa nne wa Mapinduzi ya Kiislamu kupewa jina la muongo wa maendeleo na uadilifu na kuongeza kuwa: Katika maana yake pana na ya kweli, neno maendeleo linakusanya vipengee vyote vya kimaada na kimaanawi vya mtu binafsi na jamii kiujumla ikiwa ni pamoja na uhuru, uadilifu, ustawi na kujiimarisha kiakhlaki na kimaadili, hivyo tunapaswa kushikamana na kuendelea vilivyo na njia hii ambayo Imam wetu azizi (Imam Khomeini) alituweka ndani yake.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni modeli iliyopata uzoefu na iliyofanikiwa katika suala la maendeleo na heshima ya taifa na ametoa mifano na vielelezo vya wazi vya kuonyesha maendeleo hayo ya kweli akisema: Katika kipindi cha miaka 33 iliyopita, taifa la Iran limeweza kushinda changamoto zote za kisiasa, kijeshi, kiusalama na kiuchumi zilizopangwa na kuendeshwa (na maadui) kwa lengo la kuuangamiza mfumo wa (utawala wa) Kiislamu (nchini Iran) na kwamba uhakika huu ni moja ya vielelezo muhimu sana vya ustawi na maendeleo ya taifa adhimu la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja hatua ya Iran ya kutoa taathira za wazi katika matukio ya eneo la Mashariki ya Kati na duniani kiujumla kuwa ni mifano mingine ya ustawi na maendeleo yasiyoweza kukanushika ya taifa la Iran, na huku akigusia jinsi baadhi ya viongozi na wanasiasa wa utawala wa Kizayuni wanavyoshindwa kujizuia kuukiri uhakika huo amesema: Istikama, heshima na kusimama imara taifa na mfumo (wa utawala wa Kiislamu wa Iran) katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, ni mambo ambayo yameifanya Iran kutoa taathira kubwa katika matukio muhimu ya kimataifa na ya eneo (la Masharikiya Kati).
Kazi za ujenzi na ustawi mkubwa na wa kuendelea unaoshuhudiwa katika kila kona ya Iran sambamba na kubuni na kutengeneza karakana na viwanda vinavyohitajia utaalamu mgumu na wa hali ya juu kulikofanywa na wataalamu vijana wa Iran, ni mifano mingine ya wazi ya ustawi na maendeleo ambayo imeashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake mbele ya hadhara na umati mkubwa wa watu kwenye maadhimisho ya mwaka wa 23 wa kukumbuka siku alipofariki dunia Imam Khomeini (quddisa sirruh) yaliyofanyika leo Jumapili, Juni 3, 2012, kwenye Haram ya mwanachuoni huyo mjini Tehran.
Ayatullah Udhma Khamenei, ameendelea kuzungumzia suala hilo akisema, kazi ya maendeleo na ufanifu wa kielimu nchini Iran ni kielelelezo kingine muhimu ambacho hata vituo rasmi vya takwimu dunia vimekiri kuweko kwake na amesisisitiza kwa kusema kuwa huo ni ushahidi mwingine ya kuweko maendeleo na mafanikio makubwa nchini Iran katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita.
Ameongeza kuwa: Kwa mujibu wa ripoti za kielimu za taasisi na vituo vya kimataifa, maendeleo ya kielimu nchini Iran kwa mwaka uliopita (2011) ni mara 11 zaidi ya wastani wa kimataifa sambamba na kwamba katika baadhi ya mambo kama vile nyuklia, Nano, seli shina, anga za juu na biolojia, Iran imepiga hatua kubwa sana na ina nafasi muhimu bali ni katika nchi zilizoendelea sana katika nyuga hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la demokrasia linalozidi kupata nguvu na kung'ara nchini Iran kuwa ni mfano na kielelezo kingine cha maendeleo na ufanisi wa kweli lilioupata taifa la Iran katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia suala la wananchi wa Iran kujitokeza kwa wingi na kwa hamasa kubwa katika chaguzi 10 za Rais na hasa uchaguzi wa 10 na kuanza kazi za duru 9 za Bunge bila ya kuchelewa hata kwa siku moja na kuongeza kuwa: Katika kipindi chote hiki cha miaka 33 iliyopita, hakuna tukio lolote la kisiasa, kiusalama na hata kitisho chochote kile cha kijeshi kilichoweza kukwamisha utekelezaji wa demokrasia nchini Iran.
Vile vile amekutaja kubakia hai misukumo na kaulimbiu za Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni mfano na kielelezo kingine cha mwenendo wa ustawi na maendeleo ya taifa la Iran na sambamba na kuashiria kufanyika sherehe za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa shauku na hamasa kubwa katika miaka yote hii ameongeza kuwa: Moyo wa umaanawi katika jamii nao unazidi kuimarika, tab'an katika suala hilo inawezekana baadhi ya watu wakatolea ushahidi vitendo vya baadhi chache ya watu (wasiojipamba kwa umaanawi na kusema) hivyo ndiyo hali iliyo nayo jamii nzima ya Iran, lakini watu hao wanafanya makosa, kwani kushiriki kwa wingi matabaka mbali mbali ya watu hasa vijana wa Vyuo Vikuu katika masuala tofauti ya kidini kama vile itikafu ni ushahidi wa wazi unaothibitisha kuwa harakati ya kimaanawi ya taifa la Iran inazidi kustawi.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Matukio ya uhakika tuliyoyabainisha hapa yanaonesha kuwa Iran inazidi kupiga hatua za maendeleo katika nyuga na nyanja zote, chini ya bendera ya Uislamu, chini ya kivuli cha harakati na ulinganiaji wa haki katika njia ya Mwenyezi Mungu harakati ambayo imeanzishwa na Imam wetu adhimu na kwa kutegemea moyo wa heshima ya taifa na kuimarisha muundo wa ndani wa taifa hili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, maendeleo na ustawi wa taifa la Iran sambamba na taifa hili kuwa kigezo kizuri kwa mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati na duniani kiujumla, ndiyo mambo hasa yanayowafanya maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu wajawe na hofu na woga mkubwa na kuongeza kuwa: Kitendo cha duru za kisiasa dunia cha kulikuza kupindukia suala la nyuklia la Iran na kudai ni hatari kwa Iran kuwa na nyuklia si kitu kingine zaidi ya uongo na udanganyifu kwani kitu kinachowaogopesha maadui hao si nyuklia, bali kinachowatia wahka hasa ni Iran "ya Kiislamu."
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesisitiza kuwa, Kitu ambacho kimeleta zilizala na mtetemeko kwenye misingi ya nguvu za mabeberu ni huu uhakika kwamba, taifa la Iran limeweza kuthibitisha kivitendo kuwa, inawezekana kupata ustawi na maendeleo bila ya kutegemea Marekani wala madola yaliyojaa majigambo (ya Magharibi). (Taifa la Iran limethibitisha kivitendo pia kuwa), jambo hilo linawezekana hata kwa kusimama imara na kukabiliana na madola hayo.
Vile vile amesema, Marekani na madola mengine yaliyojaa majigambo yanafanya juhudi za kuyapandikizia mataifa mengine duniani na watu muhimu na vigogo wa kisiasa wa mataifa hayo, fikra potofu kuwa, maendeleo hayawezekani bila ya kuwepo Marekani wakati ambapo taifa la Iran limethibitisha kinyume kabisa na hivyo na limetoa somo kubwa la kielimu kwa mataifa mengineyo duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa muhtasari wa maelezo yake kuhusu mifano na vielelezo vya maendeleo na ustawi wa Iran katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita na kulikhutubu taifa la Iran akiliambia: Nyinyi taifa kubwa la Iran mumefanikiwa kuweka rekodi na kupiga hatua za kimaendeleo katika kipindi hiki chote cha zaidi ya miaka thelathini, lakini kama mtajisahau na kuona maendeleo mliyopata katika kipindi hicho yanatosha, basi bila ya shaka yoyote mtafeli katika mambo yenu na mtabaki nyuma. Hivyo mnapaswa kuendelea na jitihada zenu za kujiletea maendeleo bila ya kusita hata kidogo.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja jukumu la viongozi nchini Iran katika njia ya kuelekea kwenye vilele vya juu kabisa vya ustawi, kuwa nalo ni jukumu kubwa sana na kuongeza kwamba: Katika njia hii; ni marufuku kusita na kusimama kwa namna yoyote ile, ni marufuku kujivuna na kuingiwa na ghururi, ni marufuku kujifikiria binafsi, ni marufuku kukumbwa na mghafala, ni marufuku kupenda makuu, ni marufuku kujistarehesha, ni marufuku kukusanya mapambo ya dunia, ni marufuku kutafuta umashuhuri, yote hayo ni marufuku kwa viongozi nchini na kwamba ni kwa kuchunga marufuku hizo tu ndipo itawezekana kuvifikia vilele vya juu vya ustawi.
Aidha amesisitiza kuwa: Sisi viongozi tunapaswa tujiepushe kikamilifu na magonjwa hayo yenye madhara makubwa kama ambavyo Imam wetu mtukufu aliweza kujiweka mbali na maradhi hayo hatari.
Ayatullah Udhma Khamenei amewakhutubu vijana, wanachuo, viongozi, maulamaa na watu wenye ushawishi katika jamii akisisitiza kuwa: Inabidi tuendeleze harakati yetu bila ya kusita hata kidogo kuelekea kwenye vilele vya juu ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ustawi katika masuala ya kisiasa, kisayansi na kiteknolojia na hasa maadili na umaanawi, na tuzidi kuondoa nuksani zetu katika harakati yetu hiyo.
Ameongeza kuwa, harakati isiyosita kuelekea kwenye kilele cha maendeleo itapelekea kutokuwa na athari yoyote vizuizi vinavyowekwa na adui ikiwa ni pamoja na vikwazo na ususiaji wa maadui hao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Vikwazo na ususiaji wa maadui hauwezi kamwe kulikwamisha taifa la Iran katika harakati yake inayozidi kusonga mbele bali athari pekee ya vikwazo hivyo ni kuzidi tu hasira na chuki za taifa la Iran kwa Magharibi.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbusha kuwa: Harakati ya taifa la Iran hivi sasa bado imo katika uwanda na wakati itakapofika kileleleni, basi uadui na upinzani wa kikhabithi wa maadui nao utakoma na kumalizika.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia harakati mbali mbali na mapinduzi tofauti ya wananchi yaliyoshuhudiwa katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika, kuanzia Yemen na Bahrain hadi Misri, Tunisia na Libya huku katika nchi nyingine za eneo hili, vuguvugu la harakati hizo likiwa linafukuta chini kwa chini na kusema kuwa, hiyo ni mifano ya wazi ya jinsi mataifa hayo ya Waislamu yanavyopigania heshima ya taifa, uadilifu na uhuru chini ya kivuli cha dini tukufu ya Kiislamu.
Amesisitiza kuwa: Uislamu ndani ya mwamko wa mataifa hayo ni suala lenye mizizi na misingi madhubuti na ni jambo ambalo lina ushahidi madhubuti kwani mataifa ya dunia yanapopigania uadilifu, uhuru na demokrasia hupigania kwa kuzingatia misingi na usuli za mataifa hayo na kwamba misingi ya mataifa ya eneo hili imesimama juu ya imani ya kidini ya mataifa hayo yaani imani ya Kiislamu, hivyo muundo wa harakati za eneo hili ni Uislamu na mwamko huo ni mwamko wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia njama zinazofanywa na madola ya Magharibi na tawala za Kiarabu zilizo vibaraka wa Magharibi, za kujaribu kuzipa sura nyingine harakati na mapinduzi ya wananchi katika eneo hili sambamba na kujaribu kuonesha kuwa harakati hizo hazina faida yoyote na kuongeza kuwa: Watu wenye ushawishi pamoja na wananchi wa nchi za eneo hili wanapaswa kuwa macho na makini mbele ya njama hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia pia mabadiliko makubwa katika anga ya kisiasa na kijamii ya eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika kutokana na mapinduzi ya wananchi yaliyotokea hivi karibuni kwenye nchi za eneo hili na kuongeza kuwa: Kitu ambacho tumekishuhudia hadi hivi sasa katika eneo hili ni matokeo na ni natija na mapambazuko tu na kwamba katika siku za usoni, tutashuhudia mabadiliko makubwa zaidi katika eneo hili.
Ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu mabadiliko ya kisiasa na kijamii katika eneo hili akisema kuwa: Wakati mapambano ya wananchi wa Misri yaliposhamiri na kupamba moto, Wamagharibi wengi na tawala za kidikteta za eneo hili, ziliuunga mkono utawala wa Mubarak na hatua yake ya kukandamiza wananchi, lakini baada ya wananchi wa Misri kupata ushindi (na kumng'oa madarakani dikteta Hosni Mubarak), madola hayo hayo ya kibeberu na tawala za kidikteta za vibaraka wao ambao awali walikataa kutambua haki za wananchi wa Misri, waligeuka na kuanza kuzungumzia suala la demokrasia. Amesema, jambo hilo kwa kweli linaonesha kuweko mabadiliko muhimu na makubwa katika anga ya eneo hili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja Misri kuwa ni nchi kubwa na ni taifa lenye historia kongwe na lenye ushawishi katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kuongeza kwamba, watawala fasidi na mamluki, walilifanya taifa la Misri kuwa dhalili kwa miaka mingi na waliiifanya nchi hiyo (ya Waislamu) kuwa dafina, kanzi na hazina ya kiistratijia ya utawala wa Kizayuni, lakini hivi sasa kanzi hiyo imekombolewa na kutolewa mikononi mwa Wazayuni maghasibu.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia kazi iliyokuwa imepewa serikali ya Hosni Mubarak ya kudhamini usalama wa utawala wa Kizayuni hata kwa gharama ya kuwaweka katika jela wananchi milioni moja na nusu wa Ukanda wa Ghaza huko Palestina katika mashambulizi ya kikatili ya siku 22 ya Wazayuni na kuongeza kuwa: Baada ya kuangushwa Mubarak, utawala wa Kizayuni hivi sasa unajiona uko mtupu na umeemewa na kuchanganyikiwa vibaya sana.
Vile vile ayataja makelele na vitisho vya kijeshi visivyo na lolote ndani vinavyotolewa na viongozi wa utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya Iran kuwa vinatokana na woga na kuchanganyikiwa viongozi hao na kusisitiza kwamba: Viongozi wa utawala wa Kizayuni wanajua vizuri sana kwamba, hivi sasa wako katika mazingira ya kupata madhara makubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote, na kama watachukua hatua yoyote mbovu au kufanya harakati yoyote isiyoendana na hali yao, basi watakumbwa na pigo kali mithili ya radi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameseme, hali ziliyo nayo nchi za Magharibi na Marekani hivi sasa ambao ndio waungaji mkono wakubwa wa utawala wa Kizayuni na ambao wanaunga mkono kibubusa siasa na jinai zote za utawala huo katili, kuwa ni hali mbaya na kuongeza kuwa: Leo hii kutokana na matatizo ya kiuchumi yanayoikabili Magharibi pamoja na matatizo ya kifedha na kijamii, matatizo ambayo yameziweka tawala za nchi hizo katika hali ngumu na kuzipelekea zisijue cha kufanya katika kukabiliana na wananchi, zenyewe hivi sasa zinatapatapa katika kuhakikisha zinabakia hai.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kuangushwa serikali kadhaa za barani Ulaya ambazo zilikuwa zinafuata siasa za Marekani sambamba na kuongezeka hasira za wananchi wa Ulaya dhidi ya Marekani kuwa ni mfano mwingine wa mgogoro mkubwa unaozikabili nchi za Magharibi hivi sasa.
Ameongeza kuwa, nchi za Magharibi zinajaribu kuzusha matatizo na migogoro katika mabara ya Asia, Afrika na katika eneo la Mashariki ya Kati ili kuficha mgogoro mkubwa unaozikabili nchi hizo za Magharibi.
Aidha amelitaja suala la kuzusha hitilafu za kikabila, kitaifa na kidini katika nchi za Kiislamu zilizofanya mapinduzi hivi karibuni pamoja na kujaribu kuyabadilisha mapinduzi ya wananchi hao kuwa dhidi ya wananchi wa mataifa hayo ya Kiislamu, kuwa ni mbinu nyingine zinazotumiwa na Magharibi na Marekani katika juhudi zao za kuhamishia kwengine migogoro yao.
Ameongeza kuwa: Leo hii Wamarekani wanatumia uzoefu na ile ile sifa mashuhuri ya Waingereza ya kuzusha hitilafu za kidini na kikabila - ambapo Waingereza ni mahiri sasa katika kuzusha fitna na mifarakano kama hiyo - hivyo mataifa yote, maulamaa, watu muhimu katika jamii, watu wa Vyuo Vikuu kwenye eneo hili ni sawa tu wawe Waislamu wa Kishia au Kisuni, wote wanapaswa kuwa macho na wasikubali kuwa chambo cha kufanikishia malengo hayo ya maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amevitaja vitendo hivyo vya Wamagharibi na Wamarekani kuwa ni vya kiwendawazimu na kusisitiza kuwa: Wamagharibi na Wamarekani wanajaribu kuficha mgogoro na matatizo yao na kuzishughulisha fikra za watu na masuala mengine, wanalikuza kupindukia suala la nyuklia la Iran na kujaribu kulionyesha kuwa ndilo suala kubwa zaidi hivi sasa duniani na wanaeneza maneno ya uongo kuwa eti Iran inataka kumiliki silaha za nyuklia wakati ambapo huo sio ukweli wa mambo na bila ya shaka njama zao hizo pia hazitafanikiwa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mustakbali wa eneo hili kuwa ni mtazamo wa matumaini na kuongeza kuwa: Tab'an matukio ya eneo hili yametoa fursa kwa nchi nyinginezo za eneo hili kuchukua baadhi ya hatua kwa niaba ya Marekani lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu nchi za Kiislamu zilizofanya mapinduzi na hasa Misri zitarejea katika utulivu na amani na kwamba tawala za kidikteta katika eneo hili nazo zitapinduliwa tu.
Vile vile amegusia matukio ya Bahrain na kusema kuwa, mateso wanayoyapata wananchi wa Bahrain ni makubwa maradufu.
Ameongeza kuwa: Wananchi hao wanakandamizwa na utawala wa kiimla na kidikteta bila ya sababu yoyote na upinzani wa wananchi hao unajibiwa kwa vitendo vya kikatili kabisa wakati ambapo wananchi wa Bahrain hawapiganii kitu kingine isipokuwa haki yao ya kimsingi kabisa yaani demokrasia na kuwa na maamuzi katika nchi yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, badala ya kusikilizwa matakwa ya wananchi huko Bahrani, kunafanyika njama za kulipa sura ya hitilafu za kimadhehebu suala la nchi hiyo na kulihusisha na Ushia na Usuni sambamba na kuficha matakwa halisi ya wananchi wa nchi hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, jihadi na jitihada zote zinazofanyika katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika zitafanikiwa, lakini inabidi kuwa macho na kuwa na hadhari kubwa ili kusije kukapaliliwa moto wa fitna za kikabila, kimakundi na kimadhehebu kati ya Waislamu.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Ni jambo lisilo na shaka kuwa mustakbali wa mataifa ya Waislamu na wa taifa la Iran utakuwa bora zaidi kuliko huko nyuma.



1022669
captcha