IQNA

'Nchi za Magharibi zinakasirishwa na Iran kuwa kigezo kwa mataifa mengine

18:22 - June 08, 2012
Habari ID: 2342094
Khatibu wa Sala ya Ijumaa jijini Tehran amesema kuwa hatua ya nchi nyingi kuyachukua kuwa kigezo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na ustawi wa kasi wa nchi hii katika sekta mbali mbali ndio chanzo kikuu cha mashinikizo na vitisho vya nchi za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Imami Kashani ameongeza kuwa kadhia ya nyuklia ya Iran ni kisingizio kinachotumiwa na nchi za Magharibi kuitisha na kuishinikiza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ameongeza kuwa nchi za Kimagharibi haziogopi shughuli za nyuklia zenye malengo ya amani za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bali zina wasi wasi kutokana na ushawishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika nchi zingine duniani.
Akihutubia waumini katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran, Ayatullah Imami Kashani amesema vikwazo vya Wamagharibi dhidi ya Iran ni fursa ya kujitosheleza zaidi taifa la Iran. Ameendelea kusema kuwa Wairani kamwe hawatasita kujipatia teknolojia za kisasa na kuzinasihi nchi za Magharibi zisitishe vikwazo dhidi ya Iran na badala yake zifuate sera za kimantiki. Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran ameongeza kuwa, hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuhuisha Uislamu halisi na kuandika katiba kwa msingi wa Uislamu ni jambo ambalo limeifanya nchi hii iweze kuwa na nguvu na kujitegemea. Ayatullah Imami Kashani amesema sera za kivita, utesaji mauaji, utawala wa kiimla na ukandamizaji ni baadhi ya sababu ambazo zimepelekea kuibuka mwamko wa Kiislamu. Amesema kwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, mwamko wa Kiislamu unaenea kwa kasi kote duniani.
1025093
captcha