Katika hukumu iliyotoa hapo jana mahakama hiyo imebatilisha ubunge wa thuluthi moja ya wabunge pamoja na kubatilisha sheria mpya iliyopasishwa na bunge inayojulikana kama kanuni ya kutengwa kisiasa.
Farouq Sultan, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Katiba ya Misri ametangaza kuwa kubatilishwa ubunge wa thuluthi moja ya wabunge kunamaanisha kuvunjwa bunge la nchi hiyo.
Harakati ya Ikhwanul Muslimin na vyama washirika wa harakati hiyo walikuwa na viti 127 ambavyo ni sawa na asilimia 47 ya viti vyote 498 vya bunge hilo.
Uamuzi wa Mahakama ya Katiba wa kubatilisha sheria ya kanuni ya kutengwa kisiasa iliyopasishwa na bunge umempa kibali Ahmad Shafiq, Waziri Mkuu wa mwisho wa utawala uliopita kugombea katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais. Sheria hiyo iliweka marufuku ya muda wa miaka 10 kwa viongozi wote waliohudumu katika utawala wa dikteta Hosni Mubarak ya kutoshika nyadhifa za kisiasa wala kushiriki kama wagombea katika uchaguzi.
Katika radiamali ya kwanza iliyotolewa mara baada ya kutangazwa hukumu ya Mahakama ya Katiba, wananchi wa Misri walikusanyika katika Medani ya at Tahrir mjini Cairo na kutoa kauli za kulaani hukumu hiyo. Katika kauli mbiu zao, wananchi hao waliituhumu Mahakama ya Katiba kuwa inalitii Baraza kuu la Kijeshi na wakaendelea kutilia mkazo msimamo wao wa kutaka baraza hilo livunjwe.
Aidha walitoa sisitizo la kutaka Ahmad Shafiq asiruhusiwe kugombea katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais na kutangaza kwamba wataanzisha kile walichokiita "mapinduzi mapya" ili kumzuia Shafiq asishike madaraka ya nchi. Wananchi wanamapinduzi wa Misri walifanya maandamano ya mamilioni jana mara baada ya Sala ya Ijumaa na kukusanyika katika Medani ya at Tharir kulalamikia uamuzi wa Mahakama ya Katiba wa kulivunja bunge na kuidhinisha ugombea wa Ahmad Shafiq.
Wakati huohuo baadhi ya wanaharakati wa kisiasa wa Misri wamesema hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Katiba ya kubatilisha ubunge wa thuluthi moja ya wabunge na kusababisha bunge kuvunjwa sambamba na kubatilisha sheria ya kutengwa kisiasa ni mapinduzi ya kijeshi dhidi ya mapinduzi ya wananchi.
1030875