IQNA

Rogeh Garudi aaga dunia, Chama cha an-Nahdha chatuma rambirambi

16:41 - June 17, 2012
Habari ID: 2348812
Rashid al-Ghanushi, mkuu wa chama cha Kiislamu cha an-Nahdha cha Tunisia ametoa taarifa ya salamu za rambi rambi kwa mnasaba wa kuaga dunia Rogeh Garudi, mwanafalsafa na mwandishi mashuhuri wa Kiislamu wa nchini Ufaransa.
Msomi huyo mashuhuri wa Kiislamu ambaye amekuwa akikosoa misimamo ya nchi za Magharibi kuhusiana na ulimwengu wa Kiislamu aliaga dunia siku ya Jumatano huko Paris akiwa na umri wa miaka 99.
Profesa Roger Garaudy alikuwa mhadhiri wa masuala ya falsafa katika vyuo vikuu vya Ufaransa ambapo alipata umashuhuri mkubwa duniani kutokana na msimamo wake wa kupinga madai ya Holocaust ambapo inadaiwa kuwa, mamilioni ya Mayahudi waliuawa kwa umati na Adolph Hitler huko Ujerumani.
Garaudy ambaye mwanzoni alikuwa mkomunisti mwenye misimamo mikali alihudumu katika nyadhifa mbalimbali nchini Ufaransa zikiwemo za useneta. Hatimaye alisilimu na kukubali Uislamu mwaka 1982 na kuchagua jina la Kiislamu la Raja. Msomi huyo ameacha nyuma vitabu kadhaa muhimu kikiwemo cha 'Marekani, Kinara wa Upotofu.'1031616
captcha