IQNA

Changamoto za Uturuki na uwezekano wa kukabiliana kijeshi na Syria

11:06 - June 30, 2012
Habari ID: 2356421
Kufuatia kudunguliwa na Syria ndege moja ya kivita aina ya Phantom-F4 mali ya Uturuki, inasemekana kuwa, ndege nyingine ya kivita ya Uturuki iliyokuwa katika anga ya bahari ya Mediterranean katika mipaka ya nchi mbili hizo pia imeponea chupu chupu kudunguliwa na vikosi vya jeshi la Syria.
Japokuwa tukio hilo la pili halikupelekea kuanguka kwa ndege hiyo ya Uturuki, lakini kwa mara nyingine tena suala hilo limezusha makelele na mvutano katika uhusiano wa Ankara na Damascus. Uturuki inadai kuwa, ndege iliyotajwa ilikuwa katika oparesheni ya kuwatafuta na kuwaokoa marubani wawili wa Kituruki ambao walikuwa katika ndege ya kivita iliyodunguliwa na jeshi la Syria siku chache ziliopita.
Kudunguliwa kwa ndege ya Uturuki na vikosi vya Syria ambako kumeharibu uhusiano wa pande mbili kumezusha pia mijadala na uchochezi katika vyombo vya habari kieneo na kimataifa. Vyombo vya kisiasa vya kieneo vinauliza swali hili kwamba, je, Uturuki ambayo inaegemea kwenye kipengele nambari tano cha hati ya NATO na ambayo ni mshirika wa NATO italitaka shirika hilo la kijeshi la nchi za Magharibi kuingilia kijeshi nchini Syria? Swali hili linaulizwa hasa kwa kuzingatia kuwa, huko nyuma Uturuki ililitaka shirika hilo kuishambulia kijeshi nchini Syria na sasa suala hilo limepewa kipaumbele zaidi na nchi hiyo. Tayari serikali ya Ankara imetishia kuwa, hatua iliyochukuliwa hivi karibuni na Syria ya kudungua ndege yake ya kijeshi haitapita bila kupata jibu.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, ikiwa jibu linalokusudiwa na Ankara ni hatua za kijeshi, basi ni wazi kuwa itakabiliana na changamoto nyingi. Gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung limeandika kuwa, jibu la kijeshi la Uturuki kwa Syria si tu kwamba litasababisha maafa kwa Uturuki na nchi za eneo zima la Mashariki ya Kati tu bali litakuwa mzigo mkubwa wa maafa kwa wote. Hii ni kwa kuwa, mapigano ya kijeshi kati ya nchi hizo hayatakuwa na mpaka bali yatazishirikisha NATO, Urusi na Marekani.
Ni kutokana na ukweli huo ndio maana NATO ikaitaka Ankara kuwa na subira na kutothitari vita. Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanaamini kuwa, ikiwa Uturuki itatekeleza shambulio la kijeshi dhidi ya Syria si tu kwamba itakosolewa na wananchi wa nchi hiyo tu bali na watu wote wa eneo la Mashariki ya Kati kwa ujumla. Aidha weledi wa mambo wanaamini kuwa, tabia za kijuba za Uturuki dhidi ya Syria, zimezusha hasira kali kwa wananchi wa nchi hiyo. hii ni katika hali ambayo Damascus haijawahi kuchukua hatua hasi dhidi ya Uturuki. Pia serikali ya Syria inawatuhumu askari wa kulinda amani wa Uturuki kwa kuwapa himaya magaidi wa Syria wanaokimbilia nchini humo kupitia mpaka wa pamoja wa nchi hizo. Kabla ya hapo pia serikali ya Damascus ilionyesha kusikitishwa kwake na baadhi ya nchi ikiwemo Uturuki kuwa wanawapa zana za kijeshi magaidi wanaotekeleza mauaji nchini Syria.
Hii ni katika hali ambayo duru kadhaa za Marekani na Uingereza zimekiri kuwa, Uturuki imekuwa kituo muhimu cha kutoa mafunzo kwa magaidi na wapinzani wa serikali ya Rais Bashar Al Asad wa Syria. Licha ya hayo, baadhi ya duru zimefichua kuwa, baadhi ya magaidi wa Syria wenye mafungamano na mtandao wa Al Qaida wanapata mafunzo katika nchi kadhaa za eneo hili ikiwemo Uturuki.

1038971
captcha