IQNA

Rais Mursi wa Misri anakabiliwa na vizingiti vingi

17:55 - July 01, 2012
Habari ID: 2358113
Baada ya kupita zaidi ya miezi 15 ya kuangushwa dikteta Hosni Mubarak wa Misri, wananchi wamemchagua Mohammad Mursi mgombea wa wanaotaka Uislamu kuwa rais wa nchi hiyo. Kuchaguliwa Mursi ni hatua nyingine kubwa katika kulinda mafanikio ya mapinduzi ya taifa la Misri.
Kuchaguliwa Mohammad Mursi, mgombea wa Harakati ya Ikwanul Muslimin kuwa rais wa Misri kwa mara nyingine kumethibitisha ubatili wa nadharia za Wamagharibi ambao wamekuwa wakiyataja mapinduzi ya wananchi katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika kuwa eti ni ‘Machipuo ya Kiarabu’ au Arab Spring. Kwa hivyo ushindi wa Mursi umethibitisha kuwa harakati za wananchi wa Tunisia, Misri, Libya au Bahrain zinaweza kuarifishwa tu katika fremu ya Mwamko wa Kiislamu.
‘La’ kubwa ya Wamisri kwa Ahmad Shafiq mgombea kiti cha urais ambaye alikuwa waziri mkuu wa mwisho wa dikteta Mubarak ni jambo lililoashiria kuwa Wamisri wana azma ya kukamilisha mkondo wa mapinduzi na kwamba wako macho katika harakati yao.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na ibara mbalimbali zilizotumika kutathmini matukio ya Misri. Ibara hizo ni pamoja na ‘Mapinduzi ya Pili,’ ‘Mapinduzi ya Wanajeshi’, ‘Ushirikiano wa Ikwanul Muslimin na Wanajeshi,' ‘Wamisri Wapoteza Matumaini Kuhusu Mapinduzi,’ ‘Wizi wa Kura katika Uchaguzi,‘Kurejea Mabaki ya Utawala wa Zamani, ‘Watu wataka utawala uliopita urejee,' n.k.
Lakini baada ya uchaguzi ilibainika kuwa aghalabu ya tathmini hizi hazikuwa sahihi na hili lilitokana na hamaki katika utathmini na kutoifahamu kikamilifu jamii ya Misri.
Katika zama zetu hizi, Misri imekuwa nchi muhimu katika mlingano wa kieneo. Nchi hii ilipewa lakabu ya ‘Moyo wa Ulimwengu wa Kiarabu’ kutokana na kuwa ilitoa ilhamu kwa harakati nyingi za kisiasa, kifikra na kijamii katika Ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.
Matukio yaliyojiri katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi kadhaa iliyopita na vile vile katika siku za hivi karibuni hasa ushindi wa Mohammad Morsi ni jambo linaloonyesha kuwa Misri sasa inaweza kurejea katika nafasi yake ya ushawishi katika mlingano wa kieneo na kimataifa. Misri mpya imeibuka kwa kumchagua mgombea wa Ikwanul Muslimin kuwa rais wa nchi baada ya miaka mingi ya kukandamizwa harakazi zenye mielekeo ya Kiislamu nchini humo. Nchi za Magharibi vile vile katika kipindi cha miaka 40 iliyopita zimekuwa zikiunga mkono tawala za kidekteta Misri kwa kutaja harakati za Kiislamu kuwa tishio kwa tawala vibaraka katika eneo.
Katika hali kama hii swali linalojitokeza ni je, baada ya Mursi kuchukua madaraka nchini Misri, ni yapi tutarajie katika uhusiano wa Misri mpya na nchi za eneo na dunia nzima?
Mohammad Mursi ni shakhsia anayejulikana katika jamii ya Misri. Amepata masomo ya juu kabisa ya chuo kikuu akiwa na shahada ya uzamivu katika uhandisi. Kwa hivyo anafahamika vyema katika duru za kielimu Misri. Nao wananchi wa Misri wanamfahamu kama mtu mwenye misimamo ya wastani katika siasa. Sasa swali linaloulizwa hapa ni hili kuwa je, Mursi kwa msimamo huu wake wa wastani ataweza kukabiliana na vizingiti vilivyo mbele yake na kuimarisha misingi ya mapinduzi ya wananchi wa Misri?
Changamoto muhimu zaidi aliyonayo Rais Mursi ni jeshi na watu watiifu kwa utawala wa dikteta Mubarak aliyetimuliwa madarakani ambao bado wanashikilia nafasi muhimu katika utawala wa Misri.
Joshua Stacher mhadhiri wa sayansi ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha Kent State Marekani katika makala kuhusu hali ya kisiasa Misri anasema: “Jeshi katika utawala wa Mubarak lilikuwa na ushawishi mkubwa na kwa hakika lilikuwa linashikilia madaraka. Jeshi na Ikwanul Muslimin ni taasisi mbili tafauti kabisa na kila moja ina idiolojia inayopingana na nyingine kuhusu mustakabali wa Misri.”
Nchini Misri mahakama yenye nguvu zaidi inaunga mkono jeshi. Ikumbukwe kuwa baada ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais Mahakama Kuu ya Katiba ilitangaza kuwa bunge, ambalo lilikuwa linadhibitiwa na Ikwanul Muslimin, halina msingi wa kisheria punde baada ya uamuzi huo bunge lilivunjwa. Kwa hivyo ni wazi kuwa jeshi la Misri linaweza kuvuruga urais wa Morsi na Ikwanul Muslimin kwa kutumia ushawishi wake mkubwa katika taasisi za dola.
Aghalabu ya weledi wa mambo wanatoa mfano mwingine na kusema Jeshi la Misri linadhibiti mtandao wa kusambaza bidhaa muhimu za kila siku kama vile mafuta ya petroli na petrokemikali. Iwapo jeshi litavuruga usambazwaji huo, Ikwanul Muslimin ndio itakayobebeshwa lawama zote za kisiasa.
Baadhi ya weledi wengine wanaamini kuwa moja kati ya changamoto kuu za serikali ya Mohammad Mursi ni kutoka kwa majenerali wa jeshi la polisi. Hawa ni majenerali ambao wana jukumu muhimu la kulinda usalama wa ndani na walikuwa mkono wa chuma wakati wa utawala wa dikteta Mubarak. Majenerali wenye uwezo mkubwa katika jeshi la polisi ndio ambao bado wanawasimamia vikosi vya kuzima ghasia na taasisi za kijasusi zenye nguvu kubwa.
Kwa miongo kadhaa sasa taasisi hizo za kijasusi ndizo ambazo zimekuwa zikiwakandamiza wanaharakati wa kisiasa hasa wale wa Ikwanul Muslimin. Iwapo Mohammad Mursi, kama alivyoahidi, ataamua kuisafisha serikali yake kwa kuwatimua maafisa wote wa zama za Mubarak serikalini, bila shaka atakabiliwa na upizani mkali. Ni wazi kuwa jeshi ambalo lilikuwa linamtii dikteta Mubarak litajaribu kulinda maslahi yake kwa kuvuruga juhudi za marekebisho za rais Mursi. Uvurugaji huu wa jeshi unaweza ukaathiri vibaya nafasi ya Mohammad Mursi na Ikhwanul Muslimin katika jamii.
Wakati tunapozungumza kuhusu kuja madarakani mrengo wa Kiislamu Misri, swali linalokuja haraka akilini ni kuhusu utambulisho wa uhusiano kati ya nchi hiyo ya Kiarabu na utawala haramu wa Israel. Hakuna shaka kuwa kukabiliana na utawala bandia wa Israel si katika ajenda ya Ikhwan na Rais Mursi.
Kwa kuzingatia historia ya miaka 80 ya Ikwanul Muslimin ni wazi kuwa hatupaswi kutarajia kuwa harakati hiyo itachukua mtazamo hasimu wa kukabiliana moja kwa moja na utawala haramu wa Israel. Hadi sasa hatujasikia viongozi wa Ikwanul Muslimin wakitangaza wazi wazi upinzani wao kwa Mkataba wa Camp David isipokuwa tu wametoa ahadi za hapa na pale kuhusu mabadiliko katika mkataba huo. Katika upande mwingine Morsi ametangaza bayana kuwa serikali yake itaunga mkono haki za kisheria za taifa la Palestina.
Kwa kuzingatia vizingiti vilivyoanza kuwekwa na jeshi baada ya ushindi wa Morsi, ni wazi kuwa Ikwanul Muslimin itajaribu kwanza kujiimarisha ndani ya nchi kabla ya kuchukua misimamo inayokinzana moja kwa moja na jeshi. Sera za Ikwanul Muslimin kuhusu Marekani pia zinaweza kutathminiwa kwa mtazamo huu.
Wakuu wa Ikhwan watajitahidi kuwa na uhusiano usio na utata na Marekani. Kwa uchache kile ambacho Ikwanul Muslimin inaweza kufanya ni kutounga mkono sera za Marekani katika eneo. Kilichowazi ni kuwa Ikwanul Muslimin katika stratijia yao ya muda mrefu wanataka kuiondoa Misri katika duara la waitifaki wa Magharibi katika eneo. Aidha harakati hiyo inataka Misri iwe nchi yenye sera huru za kigeni. Kwa hivyo tutasiburi tuone Morsi atachukua hatua gani kuainisha mkondo huru utakaochukuliwa na Misri katika uga wa kimataifa. Viongozi wenye mielekeo ya Kiislamu nchini Misri wanafahamu kuwa Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi zingali na ushawishi Misri.
Kwa kuzingatia hayo, inaelekea rais mpya wa Misri atajaribu kuchukua msimamo huru wenye kuleta mlingano katika sera za kigeni na wakati huo huo kulinda uhusiano na Marekani. Wakati huo huo hatupaswi kusahau kuwa wananchi wanamapinduzi wa Misri, waliomleta madarakani Mohammad Mursi, wanapinga vikali Marekani na utawala haramu wa Israel na wanatarajia kuwa Morsi atachukua muelekeo unaoenda sambamba na matakwa ya wananchi waliowengi.
1041267
captcha