IQNA

Viwanja vya ndege vya Ufaransa kuwavua hijabu wanawake wa Kiislamu

17:47 - July 01, 2012
Habari ID: 2358495
Hatua mpya ya viwanja vya ndege vya Ufaransa ya kuwavua hijabu wanawake wa Kiislamu imeamsha hasira ya Waislamu wa nchi hiyo.
Waislamu wanasema kwamba hatua hiyo ni ukiukaji wa wazi wa uhuru binafsi wa wafuasi wa madhehebu ya wachache nchini humo.
Jumuiya ya kupambana na chuki dhidi ya Uislamu ya Ufaransa CCIF ilitangaza wiki mbili zilizopita kwamba Uwanja wa Ndege wa Atlantic uliopo mjini Nantes Ufaransa umetangaza kuwa utakuwa ukiwavua hijabu wanawake wa Kiislamu na kuwalazimisha kupitia katika milango iliyo na mitambo ya X-ray kwa ajili ya upekuzi.
Kufuatia hatua hiyo wanawake wa Kiislamu wameomba waruhusiwe kuvua hijabu zao katika vyumba maalumu vilivyo na wanawake peke yao lakini ombi lao hilo limekataliwa na kutishwa kwamba iwapo watakataa kuvua na kuruhusu hijabu zao kuwekwa kwenye mashine za X-ray ima watazuiwa kupanda ndege au kukabidhiwa kwa askari usalama.
Katika kuhalalisha hatua yao hiyo iliyo dhidi ya Uislamu, askari usalama katika uwanja uliotajwa wamedai kwamba vitu vinavyohatarisha usalama vinaweza kufichwa kwenye vazi la hijabu.
Jamii ya Waislamu wa Nantes imekasirishwa na hatua hiyo ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na kumtaka Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa kushughulikia suala hilo haraka iwezekanavyo.
Kwa mujibu wa sheria za usalama za Umoja wa Ulaya maafisa wa usalama katika viwanja vya ndege vya nchi wanachama wa umoja huo hawapasi kuwalazimisha wanawake wa Kiislamu wanaopita kwenye viwanja hivyo kuvua hijabu zao. 1042066
captcha