IQNA

Mgomo wa Wapakistan wafanyika huko Quetta kulalamikia mauaji ya Mashia

17:56 - July 01, 2012
Habari ID: 2358496
Maelfu ya Wapakistan wa mji wa Quetta ambayo ni makao makuu ya jimbo la Baluchestan nchini Pakistan wamefanya mgomo wa kulalamikia mauaji ya Mashia 15 yaliyotekelezwa hivi karibuni na magaidi dhidi ya basi moja la abiria katika jimbo hilo.
Kwa mujibu wa Press TV maelfu ya wakazi, wafanyakazi na wafanyabiashara wa mji huo ulioko kusini magharibi mwa Baluchestan wamefanya mgomo huo siku moja baada ya kutokea mauaji hayo.
Vituo vyote vya biashara na idara za serikali katika mji huo zilishiriki katika mgomo huo na kufanya maombolezo ya kuwakumbuka wahanga wa tukio hilo la kigaidi.
Siku ya Alkhamisi kundi moja la magaidi lilishambulia kwa makombora basi moja lililokuwa limewabeba Mashia 40 katika eneo la Hizar Gongi katika viunga vya mji wa Quetta na kuwaua 15 kati yao huku wengine wakijerihiwa. Basi hilo lilikuwa likielekea katika mji wa Quetta kutokea nchini Iran.
Wakati huohuo viongozi wa Kishia wa Pakistan wameitaka serikali ya Islamabad kuunda tume ya uchunguzi haraka iwezekanavyo ili kushughulikia suala. Vyombo vya habari vya kuaminika vinasema kwamba katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita maelfu ya Mashia wa Pakistan wamelengwa na kuuawa na magenge ya kigaidi, hasa ya Kiwahabi nchini humo.
Kufuatia mauaji hayo mashirika ya kutetea haki za binadamu na nchi za eneo ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimelaani vikali mauaji hayo ya kiholela dhidi ya raia wasio na hatia. 1042237
captcha