Richard Falk Katibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Haki za Binadamu za Wapalestina amesema jamii ya kimataifa inatekeleza njama, pengeni kwa kutojua, dhidi ya Wapalestina.
Akihutubia kikao cha Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu mjini Geneva Jumatatu Juni pili, Falk amesema Wapalestina katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel la Ukingo wa Magharibi hawana kinga yoyote ya kisheria na kusema wanayotendewa ni ubaguzi. ‘Nafikiri tunapaswa kukiri kuhusu ukweli uliopo,’ amesema Falk huku akiulinganisha mfumo wa kisheria Ukingo wa Magharibi na wa kibaguzi na kindumakuwili na kwamba unashabihiana na mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini.
Ikumbukwe kuwa Utawala wa Kizayuni wa Israel umejenga ukuta wa kibaguzi katika maeneo ya Wapalestina huko Ukingo wa Magharibi.
Mahakama ya Kimataifa ya The Hague imeshatoa hukumu na kutangaza kuwa, ujenzi wa ukuta huo sio halali na mahakama hiyo ikautaka utawala wa Kizayuni wa Israel uandae uwanja wa kubomolewa kwa ukuta huo. Hata hivyo ujeuri wa Wazayuni na hatua ya utawala wa Tel Aviv ya kupinga hukumu hiyo na kusisitiza kwamba, mahakama hiyo haina haki ya kutoa uamuzi kuhusiana na masuala ya kisiasa, kivitendo hadi leo hukumu hiyo imeshindwa kutekelezwa.
Kwa mujibu wa mipango ya kutaka kujitanua ya Tel Aviv, Israel inataka kwa kujenga ukuta wenye urefu wa kilomita mia saba idhamini usalama wa raia wake; hata hivyo kwa mujibu wa Mahakama ya Kimataifa ya The Hague ni kuwa, kupitia ukuta huo Israel inataka kuendeleza siasa zake za kutaka kujitanua hasa mpango wake wa kupanua vitongoji wa walowezi wa Kiyahudi.
Ujenzi wa ukuta wa kibaguzi umepelekea maelfu ya hekari za mashamba ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuporwa kufuatia hatua hiyo na hivyo kuwafanya Wapalestina wengi ambao maisha yao yanategemea kilimo kukabiliwa na hatima isiyojulikana. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, himaya na uungaji mkono wa Marekani ndio unaoupa kichwa utawala huo haramu cha kuendeleza siasa zake za kinyama katika ardhi za Wapalestina. Aidha misimamo ya kidhabidhabina na isiyo madhubuti ya asasi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa na baraza lake la usalama, nayo imekuwa na nafasi muhimu katika kuufanya utawala wa Israel upate kiburi cha kuendelea kuwakandamiza wananchi madhlumu na wasio na hatia yoyote wa Palestina.
1043735