Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano kupitia afisa wake Mashariki ya Kati Bi.Ann Harrison, Amnesty imesema Rajab, sawa na wafungwa wengine wengi Bahrain wamesukumwa gerezani kwa kubainisha maoni yao kwa njia ya amani.
Suala la haki za binadamu nchini Bahrain limegeuka na kuwa maudhui muhimu kwa nchi hiyo. Ukandamizaji na mkono wa chuma wa vikosi vya usalama vya utawala wa kifalme wa Aali Khalifa dhidi ya wananchi wanaopigania haki zao za kimsingi umezifanya hata asasi za haki za binadamu ulimwenguni kupaza sauti na kulalamikia unyama huo. Shirika la Kutetea Haki za Binadamu na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa sanjari na kukosoa ukiukaji wa haki za binadamu huko Bahrain zimeutaka utawala wa Aali Khalifa kuitikia matakwa ya wananchi wa nchi hiyo. Baadhi ya nchi za Ulaya kama Ujerumani na Ufaransa sambamba na kutia saini hati iliyopasishwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhusiana na Bahrain zimeutaka utawala wa Aali Khalifa kuheshimu haki za wananchi wa nchi hiyo. Kabla ya hapo Baraza la Haki za Binadamu la Bahrain lilikuwa limetuma barua kwa asasi mbalimbali za haki za binadamu ulimwenguni ambapo mbali na kubainisha ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo, lilizitaka asasi hizo kuuchukulia hatua kali utawala wa Aali Khalifa. Ni zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu wananchi wa Bahrain walipoanzisha harakati za kudai haki zao. Katika kipindi hiki wananchi hao wamekuwa wakiandamana mikono mitupu na kutoa nara za kudai haki zao. Hata hivyo, vyombo vya usalama vya Bahrain vimekuwa vikitumia mkono wa chuma kuwakandamiza waandamanaji hao ambapo vimekuwa vikitesa na kuwanyanyasa vibaya wananchi huku vikiwatupa korokoroni baadhi yao. Hata manesi wanaowatibu majeruhi wamekuwa wakitiwa mbaroni na kuchezea vipigo. Kufukuzwa kazi wafanyakazi wa serikali kutokana na kushiriki katika maandamano ya amani limegeuka na kuwa jambo la kawaida na la kila siku la utawala wa Aali Khalifa. Katika kipindi hiki cha zaidi ya mwaka mmoja, vijana barobaro, wanawake na hata wanachuo wametiwa mbaroni kosa lao likiwa ni kuukosoa utawala wa Aali Khalifa na kushiriki katika maandamano ya amani dhidi ya utawala huo. Kama vile haitoshi, wakiwa korokoni vijana na wanawake hao hukabiliwa na mateso makubwa huku majaaliwa ya baadhi yao yakiwa hayajulikani. Pamoja na hayo, hadi sasa hakuna asasi ya kimataifa hata moja ambayo imechukua hatua za maana mkabala na jinamizi hili la masaibu ya Wabahraini. Inaonekana kwamba, ushawishi wa Magharibi na Marekani katika asasi hizo za kimataifa unafanya kazi yake. Nukta muhimu na ya kutaamali ni hii kwamba, silaha zinazotumiwa na vyombo vya usalama vya Bahrain dhidi ya wananchi zinatoka Marekani na Uingereza zinazodai kuwa vinara wa kutetea haki za binadamu ulimwenguni. Hivi sasa swali hili lingali linagonga katika vichwa vya wengi kwamba, je, ni nini falsafa ya uwepo wa Umoja wa Mataifa na asasi nyingine za kimataifa ambazo zenyewe zinajitambua kuwa watetezi wa amani, usalama na haki za binadamu? Je, kuuawa wananchi wasio na hatia wa Bahrain sio jinai? Kama haya yanahesabiwa na asasi hizo kuwa ni jinai, basi ni kwa nini hadi sasa zimepuuza sauti ya kilio cha wananchi wa Bahrain wanaotaka kusaidiwa?
1050997