IQNA

Jumuiya za kimataifa zanyamaza kimya mbele ya mauaji ya Waislamu Myanmar

10:07 - July 19, 2012
Habari ID: 2372397
Ripoti zinasema kuwa maelfu ya Waislamu wa Myanmar wameuawa katika mashambulizi yanayoendelea kufanywa na kundi la wabaguzi wa Kibudha na kwamba maelfu ya wengine wamekimbia makazi yao.
Jumuiya ya Wanafunzi nchini Iran imeitaka jamii ya kimataifa ikomeshe mauaji ya halaiki yanayofanywa na Mabudha wa Myanmar dhidi ya Waislamu waliowachache nchini humo.
Taarifa ya jumuiya hiyo imelaani kimya cha jamii ya kimataifa dhidi ya mauaji hayo ya kimbari na kusisitiza kuwa maelfu ya Waislamu wa Myanmar wanaendelea kuuawa kwa umati mbele ya macho na kimya cha jamii ya kimataifa na nchi zinazodai kutetea haki za binadamu za Magharibi.
Siku chache zilizopita pia Kamati ya Haki za Binadamu ya Vyombo vya Mahakama nchini Iran ililaani mauaji makubwa yanayofanywa dhidi ya Waislamu wa Myanmar na kusema kuwa mauaji hayo yamezidisha wasiwasi katika nchi za Kiislamu hususan nchini Iran. Kamati hiyo imesema kuwa mauaji hayo ni matokeo ya utamaduni wa nchi za Magharibi zinazopiga vita Uislamu kama vile vitendo vya kuchomwa moto nakala za Qur'ani Tukufu, kushambuliwa misikiti na kupingwa marufuku vazi la hijabu na ujenzi wa minara ya misikiti barani Ulaya.
Umoja wa Mataifa umesema kuwa ukatili wanaofanyiwa Waislamu wa Myanmar ndiyo mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika siku za hivi karibuni duniani.
Tokea mwezi Juni mwaka huu wa 2012, maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya wameuawa na makumi ya maelfu ya wengine kuachwa bila makao nchini Myanmar. 1056819


captcha