Akizungumza katika mkutano na maafisa wa Shirika la Jihadi ya Chuo Kikuu na wanachama wanaoandaa mashindano hayo ya Qur’ani yatakayofanyika katika mkoa huo, Ayatullah Mojtahed Shabestari amepongeza Shirika la Jihadi ya Chuo Kikuu kwa kujishughulisha na harakati za Qur’ani hasa kuandaa mashindano ya kimataifa ya Qur’ani ya wanachuo Waislamu.
Amesema utamaduni bora zaidi ni utamaduni wa Qur’ani Tukufu na ametoa wito wa kufanyika utafiti kuhusu mafundisho ya Qur’ani Tukufu.
Ayatullah Shabestari ambaye pia ni Imamu wa Sala Ijumaa mjini Tabriz amesema mashindano hayo ya Qur’ani yaliyopangwa kufanyika mjini humo kati kati ya mwezi Septemba yatakuwa katika wakati mzuri ambao tunashuhudia mwamko wa Kiislamu duniani.
Akizungumza katika kikao hicho, mkuu wa Shirika la Jihadi ya Chuo Kikuu Mohammad Hussein Yadegari amesema shirika hilo linafuatialia kwa karibu utekelezwaji programu za Qur’ani Tukufu.
Aidha ameongeza kuwa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur’ani lenye makao yake nchini Iran sasa linasambaza habari za Qur’ani kwa lugha 40.
Naye Mkuu wa Shirika la Shughuli za Qur’ani la Wanachuo wa Iran ambaye pia ni katibu wa Mashindano ya 4 ya Kimataifa ya Qur’ani ya wanachuo Waislamu Hujatul Islam wa Muslimin Sayyed Mahdi Taqavi amesema mashindano hayo yamepata hadi kubwa duniani. Ameelezea matumaini yake kuwa mashindano hayo yataweza kubainisha masuala kadhaa hasa kuhusu mwamko wa Kiislamu.
1057714