IQNA

Mkuu wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kisuni ya Ufaransa awa Mshia

15:42 - July 25, 2012
Habari ID: 2377483
Sheikh Sanko Muhammadi, Mkuu wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kisuni ya Ufaransa amejiunga na madhehebu ya wafuasi wa Ahlul Beit (as) yaani Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw).
Sheikh huyo aliye na umri wa miaka 68 amechukua hatua hiyo akiwa safarini katika mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraqi.
Kwa mujibu wa televisheni ya Press TV, sheikh huyo mara tu baada ya kutangaza kuukubali Ushia ameelezea masikitiko yake makubwa kutokana na kuwa hakufanikiwa kuijua madhehebu hii ya Ahlul Beit (as) kwa muda wote wa maisha yake. Amesema baada ya kuona mwanga wa ukweli wa madhehebu ya Shia sasa atatumia umri wake wote uliobaki kueneza mafundisho ya madhehebu hii duniani.
Sheikh Sanko Muhammadi amesema amefanikiwa kuutambua ukweli baada ya kuzuru na kuyatembelea makaburi ya kizazi cha Mtume (saw) huko Karbala. Amesema ameamua kuutembelea mji huo mtakatifu ili ajue ukweli wa mambo ambao baadhi ya watu wanadhani wanaweza kuuficha. Ameendelea kusema kuwa sasa nafsi yake imekuwa huru na tulivu kufuatia utambuzi wake wa ukweli na kuwa atakuwa askari shupavu wa kupigania haki na mafundisho ya Ushia.
Sheikh Sanko ambaye asili yake ni Mcameroon ameishi kwa miaka 43 nchini Ufaransa na sasa ni raia wa nchi hiyo. Yeye ni Imamu wa jamaa na mkuu wa Kituo cha Fatuwa cha Ufaransa na amekuwa na nafasi muhimu katika ujenzi wa misiki katika nchi za Ulaya. 1062009
captcha