Kufuatia kuakisiwa habari zinazohusiana na mauaji yanayotekelezwa na utawala wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo na vilevile watu 80,000 kufukuzwa katika nyumba zao kufuatia mauaji hayo, Navi Pillay Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa amri ya kuchunguzwa mauaji hayo.
Kwa mujibu wa tovuti ya On Islam, afisa huyo mkuu wa masuala ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa amesema hatua yake hiyo imechukuliwa kutokana na kuwa kuna ripoti nyingi zinazotolewa na vyombo huru vya kuamini kuhusiana na ubaguzi, jinai na mauaji yanayofanywa na askari usalama wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.
Pillay amesema anaamini idadi ya Waislamu waliouawa katika mkoa wa Rakhine nchini Myanmar ni kubwa kuliko ile inayoakisiwa na vyombo vya habari na kwamba sasa anafanya mashauriano na viongozi wa nchi hiyo ili kutuma nchini humo mjumbe wake maalumu atakayechunguza kwa karibu suala hilo.
Umoja wa Mataifa umesema kwamba Waislamu hao wachache ambao asili yao ni Bangladesh na wanaojulikana kwa jina la Rohingya wanaishi katika mazingira ya kusikitisha sana kimaisha kutokana na dhulma pamoja na ubaguzi wanaofanyiwa na Mabudha waliowengi pamoja na serikali ya Myanmar.1065179