IQNA

Hali nchini Saudi Arabia yazidi kuwa mbaya

17:04 - July 31, 2012
Habari ID: 2381534
Sambamba na kushadidi malalamiko na maandamano dhidi ya utawala wa Kifalme wa Aali Saud nchini Saudi Arabia katika majuma ya hivi karibuni, gazeti moja la nchini humo limeripoti habari ya kuongezeka umaskini, ukosefu wa ajira na ufisadi nchini.
Imeelezwa kuwa, mambo hayo ni hatari na changamoto kubwa kwa utawala wa nchi hiyo. Gazeti la Okaz mbali na kuelezea kuvurugika usalama, kulegalega hali ya kisiasa na kuzorota uchumi wa nchi hiyo limeripoti kwamba, Saudi Arabia inajipatia pato la zaidi ya dola bilioni 400 kwa mwaka kutokana na kuuza mafuta, lakini licha ya utajiri huo, zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wake wanaishi chini ya mstari wa umasikini.
Takwimu zinaonyesha kwamba, kipato cha mwananchi wa kawaida wa Saudia ni chini ya dola mia nne. Umasikini na ukosefu wa ajira unazidi kupanuka nchini Saudia katika hali ambayo, wananchi wa nchi hiyo wanaaamini kwamba, maelfu ya watoto wa familia ya Kifalme wamekuwa wakipora utajiri wa kitaifa wa nchi hiyo kwa ajili ya kujiandalia maisha ya anasa na starehe ndani na nje ya nchi hiyo.
Abdul Azizi al-Khamis mwandishi wa Kisaudia ameashiria takwimu zinazokinzana za viongozi wa Riyadh kuhusiana na kiwango cha ukosefu wa ajira na kusema kuwa, kwa mujibu wa utafiti wa wachumi wa kujitegemea wa Saudia, kiwango cha ukosefu wa ajira nchini humo kimeongezeka kwa asilimia 36. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mtandao wa masuala ya kazi wa Bayat, zaidi ya raia milioni moja, laki moja na ishirini na nne elfu hawana ajira nchini Saudia. Ripoti nyingine zinaonyesha kwamba, takribani asilimia 40 ya wananchi wa Saudia ni masikini huku asilimia 70 wakiwa hawana uwezo wa kumiliki nyumba.
Si hayo tu, bali asilimia hiyo haina huduma za chini kabisa za elimu. Kwa msingi huo inawezekana kusema kuwa, licha ya Saudi kupata pato kubwa kutokana na kuuza mafuta, wananchi wa nchi hiyo wangali wanataabika na umasikini huku kiwango cha ukosefu wa ajira kikiongezeka kila siku kama wanavyokiri viongozi wa Riyadh wenyewe.
Kwa mujibu wa ripoti za duru za Saudia, ni makosa kudhani kwamba, akthari ya wananchi wa nchi hiyo wana nyumba na magari ya kutembelea; kwani uhakika wa mambo ni kuwa, akthari ya wananchi hao hawamiliki hata nyumba ya kuishi. Hii ni katika hali ambayo, wana wa kifalme wanadhibiti milki, mali na asasi zote za serikali na zile za binafsi. Fauka ya hayo wamerundika mabilioni ya dola katika mabenki ya Magharibi, fedha ambazo kimsingi ni mali ya wananchi wa Saudi Arabia.
Katika upande mwingine Kama tunavyoshuhudia, Saudi Arabia hivi sasa inapitia katika siku zilizojaa misukosuko. Matukio ya hivi karibuni mashariki mwa Saudia na kuongezeka maandamano ya wananchi katika eneo hilo ni kengele ya hatari kwa utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Saud. Waandamanaji wamekuwa wakitoa nara za kutaka mabadiliko katika mfumo wa kisiasa unaotawala Saudi Arabia.
Aidha wametoa nara za kutaka kuangusha utawala wa ukoo wa Aal Saud. Katika siku za hivi karibuni miji ya Qatif na Awamiyyah huko mashariki mwa Saudia imegeuka na kuwa medani ya maandamano makubwa ya wananchi wanaotaka utawala wa Aal Saud upinduliwe. Maandamano hayo yamevamiwa na kushambuliwa na vikosi katili vya kijeshi ambapo watu kadhaa wameuawa shahidi na wengine kujeruhiwa vibaya.
Kati ya waliojeruhiwa ni Sheikh Nimr Baqir an Nimr mwanazuoni maarufu wa Kishia nchini Saudia ambaye tayari ameshatiwa mbaroni na vikosi vya usalama. Kutiwa nguvuni mwanzuoni huyo kumepelekea kuongezeka machafuko mashariki mwa Saudia na wananchi wameazimia kukabiliana vilivyo na watawala madhalimu.
Imebainikwa kuwa watawala wa Saudia wameingiwa na wasi wasi mkubwa sana kutokana na machafuko hayo. Kile wanachoogopa ni kuenea mwamko wa mashariki hadi maeneo yote ya Saudi Arabia.
Kwa kuzingatia hilo eneo la mashariki mwa Saudia sasa limeanza kutawaliwa kijeshi ili kudhibiti hali ya mambo.
Imedokezwa kuwa watawala wa ukoo wa Aal Saud wameazimia kutuma wanajeshi zaidi ya elfu tatu katika eneo la mashariki linaloshuhudia machafuko. Aidha wanajeshi wote wa Saudia waliokuwa likizoni wametakiwa kurejea kazini mara moja na sasa wako katika hali ya tahadhari huku wakijitayarisha kuelekea katika miji ya Qatif na Awamiyyah.
Kati ya vikosi vitakavyotumwa mashariki mwa Saudia ni vile vila 'Gadi ya Taifa' ambavyo vinasimamiwa na mwanamfalme Mutaib bin Abdulaziz Aal Saud. Lengo la kutumwa vikosi hivyo katika eneo la mashariki ni kujaribu kukandamiza mwamko wa wananchi. Lakini suali linalojitokeza hapa ni hili, je, sera za kutumia mabavu na silaha zinaweza kuzima kilio cha watu wanaopigania haki na uhuru?
Saudi Arabia inaendeshwa kwa mfumo wa kale wa kisiasa uliojengeka kwa msingi wa utawala wa kiimla wa ukoo mmoja wa Aal Saud unaosimamia kila kitu nchini humo. Mfumo huo wa kiimla umejengeka katika misingi ya taasubi za kimadhehebu za kundi la walio wachache. Suala hili limekuwa likipingwa kwa miaka mingi lakini sauti za wanyonge wanaopigania uadilifu zimekuwa zikizimwa kwa mkono wa chuma wa ukoo wa Aal Saud.
Lakini hivi sasa hali ya ndani ya Saudia imeathiriwa na Mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa katika katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika. Kwa kuzingatia hilo, ukoo wa Aal Saud umeingiwa na kiwewe na umeamua kutumia nguvu za kijeshi kukandamiza mwamko wa wananchi.
Lakini uzoefu unaonyesha kuwa kutumia nguvu za kijeshi hakutakuwa na natija nyingine ila kuimarisha irada ya wananchi ya kupigania haki zao. Ni wazi kuwa misingi ya ukoo wa Aal Saud imetikisika na hatima yake itakuwa sawa na ya madikteta wengine katika eneo hili ambao wanaanguka mmoja baada ya mwingine.
1065978
captcha