IQNA

Kiongozi Muadhamu aonana na magwiji wa lugha

22:25 - August 05, 2012
Habari ID: 2386247
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameonana na malengo, magwiji wa lugha na fasihi ya Kifarsi na washairi vijana, katika hafla iliyofanyika kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa "Karimu Ahlul Bayt" Imam Hasan al Mujtaba AS.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria katika mkutano huo kuwa, msafara wa fani ya ushairi nchini Iran unaendelea kwa kasi na safari yake tena kwa umakini na muelekeo sahihi na kuongeza kuwa, iwapo harakati hiyo itaendelea vivi hivi na kwa kasi hii hii, basi Iran azizi kwa mara nyingine itaweza kuutunuku ustaarabu na utamaduni wa mwanadamu duniani, zawadi nyingine yenye thamani kubwa, na hasa katika eneo la Mashariki ya Kati.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, sambamba na kwamba fani ya tungo za kishairi ni fursa ya kuweza kubainisha hisia za washairi, lakini pia fani hiyo inabidi itumikie mambo matukufu; na katika kutekeleza majukumu yake kutokana na neema hiyo adhimu aliyobarikiwa na Mola wake, mshairi anapaswa wakati wote aitumikie dini, maadili, Mapinduzi na kuongeza maarifa ya watu kupitia tungo zake.
Ameongeza kuwa, fani ya ushairi inaweza kuwasaidia sana watu katika kupata maarifa ya kidini na kujipamba kwa maadili bora kama ambavyo pia inaweza kusaidia katika harakati ya kimapinduzi ya taifa. Amesisitiza kuwa, hilo linawezekana hata kwa beti moja au mbili tu za shairi la kimapinduzi, kiakhlaki, kimaadili na lililobeba madhumuni makubwa yaliyojaa mafunzo na maarifa.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia umuhimu wa kuzingatiwa misingi mitatu mikuu katika utunzi wa tungo za kishairi na kutaja misingi hiyo kuwa ni kuteua maneno sahihi, kuzingatia maudhui iliyo bora na kuwa na dhuku na hisia bora za kishairi. Amesema, kazi za kishairi haziwezi kufumbia macho wala kudharau masuala yanayojiri kila leo nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja dhulma kubwa linayofanyiwa taifa la Iran na madola ya kibeberu katika kadhia yake ya nyuklia ikiwa ni pamoja na kuuliwa wanasayansi na wataalamu wake bora kuwa ni miongoni mwa masuala muhimu ambayo mshairi hawezi kuyafumbia macho.
Amebainisha pia kuwa, kambi ya kiistikbari imesimama wima kukabiliana na taifa la Iran kwa nguvu zake zote za kipropaganda, kisiasa na ukhabithi wa kila namna, lakini taifa la Iran nalo linaendelea kupambana kiume na linaendelea na muqawama wake mbele ya uadui huo wa mabeberu. Amesisitiza kuwa, kadhia hii inayolihisi taifa zima, haipaswi kufumbiwa macho na washairi walio makini na wanaoheshimu fani zao kwani haiwezekani kwa mtu kutokuwa na msimamo wowote mbele ya mapambano ya haki na batili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia namna baadhi ya watu wanaodai kupigania utaifa walivyolidharau suala la vita lilivyolazimishwa taifa la Iran kupigana (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Iran) na kuongeza kuwa, watu hao ambao wanafanya propaganda za kueneza fikra za kujihusisha na mambo ya kipuuzi, dharau na kutojali mafundisho ya kidini wala kimaadili na wala masuala ya kimsingi na ya kimapinduzi nchini, ndio hao hao ambao hawaonyeshi hisia zozote mbele ya adui wa kigeni anapoivamia nchi.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametoa nasaha akisema: Watu ambao wanatumia rasilimali yao ya sanaa katika kambi ya haki na umaanawi, wanapaswa kuwa macho wakati wote, na daima wasimame kidete na wawe imara kikamilifu katika njia yao hiyo ya haki.
Mwanzoni mwa hafla hiyo, malenga kadhaa wamesoma mashairi yao ya kidini, kijamii na kimapinduzi ikiwa ni pamoja na tungo zilizohusiana na mwamko wa Kiislamu.
1070961
captcha