Kwa mujibu wa gazeti la al-Quds al-Arabi linalochapishwa mjini London, ripoti hiyo imetolewa na Martin Nesirky, msemaji wa Ki-Moon ambaye amelaani mauaji hayo akiyataja kuwa ni ya kutisha.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelezea hasira yake katika taarifa ya kulaani mauaji hayo akisema kuwa inasikitisha kuona kwamba mauaji hayo yanafanyika kwa misingi ya kutovumiliana kiitikadi. Pia ametoa salumu zake za rambirambi kwa familia ya wahanga wa tukio hilo la kigaidi.
Kwa msingi wa ripoti hiyo, Siku ya Alkhamisi iliyopita watu waliokuwa na silaha walishambulia basi moja la abiria katika eneo la kaskazini magharibi mwa Pakistan na kuwateremsha watu wote waliokuwemo na kisha kuwaua kinyama na kuwajeruhi wengine kwa kuwapiga risasi kwa karibu. Abiria hao walikuwa wakitokea Rawalpindi kulekea katika mji wa Galgut ambao ni mji wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Siku hiyohiyo Mashia wengine watatu waliuawa na magaidi katika mji wa Quetta katika jimbo la Baluchestan kusini magharibi mwa Pakistan.
Kufuatia mauaji hayo ya kinyama dhidi ya watu wasio na hatia mamia ya wananchi wa Pakistan wamefanya maandamano makubwa katika mji wa Karachi ulio kusini mwa nchi wakilaani mauaji ya kiholela yanayofanywa na magaidi wa Kiwahabi dhidi ya Waislamu wa Kishia nchini humo. 1081350