Kwa kujibu wa utangulizi wa azimio la mkutano huo, mkutano ujao wa jumuiya hiyo utafanyika nchini Venezuela.
Azimio la mwisho la mkutano huo limeunga mkono miradi ya nyuklia ya Iran inayofanyika kwa malengo ya amani sambamba na kulaani vikwazo vya Wamagharibi dhidi ya Tehran na kuunga mkono kwa sauti moja haki za taifa la Palestina.
Vilevile imetetea haki ya kila nchi ya kustawisha, kuzalisha na kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya kiraia bila ya kuwepo ubaguzi wa aina yoyote. Imepinga uzalishaji, kumiliki na kusasisha silaha za nyuklia na kusema kuwa silaha hizo ni tishio kubwa la mwanadamu.
Pia harakati ya NAM imetoa wito wa kutokomezwa silaha za nyuklia na kukosoa mipango ya nchi za Magharibi ya kusambaza fikra za chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi kote ulimwenguni.
Taarifa ya mwisho ya mkutano wa NAM mjini Tehran pia imesisitiza juu ya udharura wa kuanzishwa mfumo mpya wa uendeshaji wa masuala ya kimataifa wenye insafu, uadilifu na utakaozishirikisha nchi zote katika kukabiliana na changamoto mbalimbali na vitisho vya kiusalama, hatari zinazokabili mazingira, mabadiliko ya hali ya hewa, suala la wahajiri, maradhi ya kuambukiza, na masuala ya kiuchumi.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa ubaguzi wa kizazi ni kuvunjia heshima utukufu wa mwanadamu na usawa wa binadamu. Imesema aina mbalimbali za ubaguzi wa kizazi na jinai zinazohusiana na suala hilo katika maeneo mbalimbali ya dunia vinatia wasiwasi. Kwa msingi huo kuna udharura wa kuchukuliwa hatua madhubuti na kuwa na azma na irada ya kisiasa ya kushughulikia sura na vielelezo vyote vya ubaguzi wa kizazi, tabia ya kuwapiga vita wageni, kuwaogopesha watu kuhusu dini ya Uislamu na kadhalika, utumwa na sura zake zote mpya na magendo ya binadamu.
Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mwishoni mwa mkutano huo kwamba viongozi wa NAM wamesisitizia suala la kufanyiwa marekebisho mfumo wa kuendesha masuala ya dunia na kukabiliana na maamuzi ya upande mmoja na siasa za kupenda kujitanua baadhi ya nchi duniani. 1088704