Tovuti ya AllAfrika imeripoti kuwa, wakazi wa jimbo la Katsina wamefanya maandamano makubwa katika mitaa ya makao makuu ya jimbo hilo wakipiga nara zinazopinga siasa za Marekani na kuchoma moto bendera za nchi hiyo. Waandamanaji hao wamelaani vikali vitendo vya kuvunjiwa heshima matukufu ya Uislamu na waungaji mkono wake huko Marekani.
Kiongozi wa maandamano hayo Othman Muhammad ameviambia vyombo vya habari kwamba maandamano hayo yamefanyika kwa lengo la kudhihirisha hasira na malalamiko ya Waislamu dhidi ya watengenezaji wa filamu hiyo chafu inayokusudia kuchafua sura safi na takatifu ya Mtume Mtukufu (saw).
Ameongeza kuwa Mtume Muhammad (saw) ana nafasi ya kipekee na takatifu kwa Waislamu wote na kwamba wafuasi wa dini hiyo wako tayari kusabilia roho zao kwa ajili ya kumtetea mtukufu huyo.
Abu Bakar Ahmad Raja ambaye ni miongoni mwa washiriki katika maandamano hayo amesema kuwa umefika wakati sasa kwa walimwengu kuheshimu dini ya Uislamu kwani Waislamu wamekuwa wakiheshimu dini za watu wengine. 1098782