IQNA

Marekani yautusi Uislamu na kunufaika na hasira za Waislamu

23:11 - September 16, 2012
Habari ID: 2412475
Hakuna shaka kuwa Marekani ilikuwa ikifahamu kwamba uvunjaji heshima wowote dhidi ya matukufu ya Waislamu unatosha kuamsha hasira zao. Hata hivyo suala hilo limetokea, na ni karibu siku tano sasa ambapo ulimwengu wa Kiislamu umeshikamana na kuonyesha upinzani wake dhidi ya Marekani.
Ni wazi kwamba Ijumaa ya juzi tarehe 14 Septemba tunaweza kuiita ‘Ijumaa ya hasira za umma wa Kiislamu dhidi ya Marekani’. Viongozi wa Washington ndio walioanzisha njama dhidi ya Waislamu kwa kushirikiana na Wazayuni. Wao ndio waliochochea moto huo na hivi sasa pia wanataka kunufaika na hali hiyo kwa ajili ya maslahi yao katika eneo. Ripoti mbalimbali zinaeleza pia juu ya njama za Marekani za kutaka kuimarisha vikosi vyake katika baadhi ya nchi za Kiarabu kwa kisingizio cha kuzilinda balozi zake katika nchi hizo.
Kuwasili wanajeshi wa Marekani 150 huko San'aa mji mkuu wa Yemen, kuanza safari za manowari mbili za Marekani zilizobeba makombora ya Tom Hawk kuelekea katika maji ya Libya na kupaa ndege mbili za Marekani zisizo na rubani katika anga ya Libya, yote hayo yanadhihirisha njama mpya zinazotekelezwa na Marekani katika eneo.
Nukta muhimu hapa ni kwamba George Little msemaji wa Pentagon ameitaja hatua ya Marekani ya kutuma wanajeshi hake huko Yemen na Libya kuwa ni katika hatua ya Washington ya kujilinda. Viongozi wa Marekani wameamua kutuma wanajeshi wa nchi hiyo katika nchi za Kiarabu kwa kisingizio cha kufanyika maandamano dhidi ya nchi hiyo katika nchi za eneo na kwamba balozi na maisha ya wanadiplomasia wa nchi hiyo yako hatarini, suala ambalo Washington ilishalifikiria tangu huko nyuma.
Ni wazi kuwa Marekani ilishirikiana na shirika la kijeshi la NATO wakati wa mapinduzi huko Libya, hata hivyo Washington imekuwa ikitafuta kisingizio tu ili kuweza kuwa na nafasi na ushawishi nchini humo sambamba na kuanza awamu mpya huko Libya.
Kuonyeshwa filamu inayomvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu (s.a.w) katika ukurasa wa You Tube kitendo ambacho kimeamsha hasira za Waislamu kote duniani na kuwapelekea wananchi wa Libya kuushambulia ubalozi mdogo wa Marekani katika mji wa Benghazi nchini humo na kusababisha vifo vya balozi na wanadiplomasia kadhaa wa Marekani, kumetoa fursa kwa viongozi wa White House kutuma wanajeshi zaidi huko Libya kwa kisingizio cha kuwalinda wafanyakazi wa ubalozi wake nchini humo.
Si huko Libya pekee, bali viongozi wa Washington wamekuwa wakiikodolea jicho la tamaa Yemen pia kutokana na kuwa kwake karibu na lango bahari la kiistratejia la Babul Mandab, na kuwa njia ya kimataifa ya baharini na sehemu muhimu ya njia za meli.
Marekani ambayo kipindi fulani ilituma wanajeshi wake huko Yemen kwa kisingizio cha kupambana na harakati za mtandao wa al Qaida na vitendo vya ugaidi hivi sasa imeamua kutuma wanajeshi wake nchini humo ikiwa na lengo lingine kwa kudai kwamba inakabiliwa na wimbi la harakati zilizo dhidi yake.
Hii ni katika hali ambayo Marekani hivi sasa pia imeanzisha makelele ya kipropaganda katika eneo lengo likiwa ni kuzusha mgogoro mpya na kuzipotosha fikra za waliowengi kuhusu siasa zake katika kuamiliana na baadhi ya nchi zikiwemo Syria na vile vile kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani. Hata kama hii si mara ya kwanza kwa Marekani na Magharibi kuyavunjia heshima matukufu ya Waislamu, lakini kuchaguliwa kipindi hiki kwa ajili ya kutekeleza kitendo hicho cha dharau ambapo ilifahamika tangu mwanzo kuwa kingekuwa na athari gani, ni mpango ulioratibiwa.
Inachofanya Marekani leo hii ni kama ilivyokuwa katika miaka tisa iliyopita wakati ilipoishambulia kijeshi Iraq, ambapo ilihalalisha kuweko kwake kijeshi nchini humo kwa madai kuwa imetekeleza mashambulizi hayo kwa lengo la kujilinda. Katika siku za hivi karibuni nchi za eneo la Mashariki ya Kati zimeshuhudia maandamano dhidi ya Marekani, lakini huko Libya na Misri hali ya mambo ilikuwa tafauti. Huko Libya balozi wa Marekani na wanadiplomasia kadhaa wa nchi hiyo waliuawa. Kitendo hicho kinatosha kuifanya Marekani ipate kisingizio cha kufikia lengo lake la kutaka kuweko kijeshi huko Libya.
Viongozi wa White House wanahisi kwamba iwapo Marekani itaweza kuwa na nafasi au kuweka vituo vyake vya kijeshi huko Libya, hatua hiyo itakuwa sawa na kufanikiwa kuongoza na kudhibiti hali ya mambo ya baadhi ya nchi za Kaskazini mwa Afrika ikiwemo Misri pia.
Kwa kuzingatia uhakika huo tunaweza kusema kuwa kitendo kilichofanywa na Marekani cha kumtusi Mtume Muhammad (s.a.w) si tu kuwa kinaonyesha uadui wa wazi wa viongozi wa nchi hiyo dhidi ya Waislamu, bali kimetekelezwa ili kuandaa mazingira kwa ajili ya kuweko wanajeshi zaidi wa Marekani katika eneo na hasa katika nchi za Kiarabu ambazo zinapitia tajiriba ya kipindi kipya baada ya kujiri mapinduzi ya wananchi katika nchi hizo.

1098721
captcha