Dakta Ali Akbar Velayati, mshauri wa Kiongozi wa Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesema Washington inalitumia kundi la Munafiqina ili kufidia kushindwa kwake katika eneo na kuweza kufanikisha malengo yake ya kibeberu. Amesema hatua hiyo inaonyesha jinsi Marekani ilivyoingia kwenye mkwamo na kugonga mwamba katika kufikia malengo yake katika Mashariki ya Kati. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza siku ya Ijumaa kuwa nchi hiyo imeliondoa kundi la Munafiqina, maarufu kama MKO kwenye faharasa yake ya makundi ya kigaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo uamuzi huo umechukuliwa kwa sababu kundi hilo halijafanya shambulio lolote la kigaidi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Kwa hakika ni kipimo cha dhihaka na cha kuchekesha kilichotumiwa na serikali ya Washington kuamua kwamba hata kama mtu atakuwa ameua maelfu ya watu au kuamuru kuuawa watu hao, lakini baada ya muda kupita huwa hana hatia tena kwa jinai alizotenda.
Marekani inaliunga mkono kundi la Munafiqina ambalo inadai halijahusika na shambulio lolote la kigaidi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita katika hali ambayo ndani ya kipindi hicho, kama ulivyofanya utawala wa Baath wa Sadddam nchini Iraq, Washington nayo imelitumia kimaslahi kundi hilo ili kufikia malengo yake. Katika miaka ya karibuni Marekani imewatumia na kushirikiana na nao maajenti wa kundi la kigaidi la MKO katika operesheni za hujuma na za kijasusi dhidi ya Iran.
Washington aidha inadai kwamba kutokana na kuhamishwa wanachama wa kundi la kigaidi la Munafiqina katika kambi ya Ashraf mkoani Diyala nchini Iraq sambamba na kupokonywa silaha, kundi hilo halitojishughulisha tena na vitendo vya kigaidi na kwa hivyo hakuna sababu tena ya kuliweka kwenye orodha ya makundi ya kigaidi.
Hii ni katika hali ambayo nyaraka na ushahidi madhubuti uliopo unaonyesha kuwa tangu mwaka 1980 wakati MKO iliposhirikiana bega kwa bega na utawala wa Saddam katika vita ulivyoanzisha dhidi ya Iran, Washington imekuwa ikilitumia na kuliunga mkono kila mara kundi hilo katika hujuma zake dhidi ya Iran.
Mauaji ya kigaidi ya wanasayansi wa nyuklia wa Iran ni mfano hai wa ushirikiano wa serikali ya Marekani, maajenti wa shirika la ujasusi la Israel Mossad, na kundi la Munafiqina dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ripoti ya karibuni ya gazeti la Kizayuni la Yediot Ahronot imethibitisha jambo hilo kwa kuandika kuwa uamuzi wa Marekani wa kuliondoa kundi la Munafiqina katika orodha ya makundi ya kigaidi ni zawadi ya Washington kwa kundi hilo kutokana na mashirikiano liliyotoa kwa maajenti wa Mossad katika operesheni za kuhujumu miradi ya nyuklia ya Iran.
Kufutwa jina la MKO katika orodha ya makundi ya kigaidi ya Marekani sambamba na uungaji mkono wa Washington kwa magaidi nchini Syria kwa hatua yake ya kuutumia kimaslahi mtandao wa kigaidi wa al Qaeda kuwaua raia wasio na hatia wa nchi hiyo kunadhihirisha jinsi Marekani ilivyo tayari kuunga mkono kwa maslahi yake ugaidi ulioratibiwa kwa kalibu na sura tofauti.
Bado haijasahaulika kuwa Marekani ilileta majeshi yake katika eneo la Mashariki ya Kati ili kupambana na ugaidi wa mtandao wa al Qaeda, lakini ili kuiangusha serikali ya muqawama ya Syria iliyoko mstari wa mbele katika kukabiliana na ugaidi wa kiserikali wa Israel, leo hii Washington imeamua kutuma wapiganaji wa al Qaeda huko Syria na kuutumia ugaidi huohuo kwa ajili ya kufikia malengo yake haramu.
Hatua ya kuliondoa kundi la Munafiqin kwenye orodha ya makundi ya kigaidi nayo pia inaweza kutathminiwa kwa mtazamo huohuo huku Washington ikilenga kulitumia kundi hilo katika kalibu na sura nyengine ili kufanikisha malengo yake ya kibeberu dhidi ya Iran.
1109992