IQNA

Imam Khamenei: Utukufu wa taifa la Iran ndio sababu ya vikwazo

15:11 - October 11, 2012
Habari ID: 2429795
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Wamagharibi wanashadidisha vikwazo vyao dhidi ya Iran kutokana na taifa hili kulinda utukufu wake na kuwa na irada imara ya kujitegemea.
Kiongozi Muadhamu ameyasema hayo leo katika hadhara ya maelfu ya wakazi wa mkoa wa Khorasani Kaskazini, ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Akibainisha kuwa, vikwazo si suala geni kwa Iran katika kipindi chote hiki cha miaka 33 iliyopita, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema, Marekani na Ulaya zinaliwekea vikwazo taifa hili kwa kisingizio cha eti msimamo wa Iran kuhusiana na miradi yake ya nyuklia, lakini kwa hakika madai hayo ni urongo mtupu, kwani vikwazo hivyo vilianza hata kabla ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuanza shughuli zake za nyuklia zenye malengo ya amani. Ameongeza kuwa, vikwazo hivyo havina maana na kwamba vinatekelezwa kwa misingi ya chuki na kinyongo cha maadui na kusisitiza kuwa, maadui hao wanasema urongo wanapodai kuwa, ikiwa taifa la Iran litasimamisha miradi yake ya nyuklia eti nao watasimamisha vikwazo hivyo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kile kinachowatia kiwewe na hamaki Wamagharibi ni msimamo, utukufu na irada imara ya kujitegemea taifa la Iran ambalo limeyafikia hayo kwa baraka za Uislamu na Qur'ani tukufu. Akiashiria kuwa, maadui wana chuki na dini tukufu ya Kiislamu na shakhsia adhimu ya Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) sambamba na kumvunjia heshima mtukufu huyo amesema, maadui wanayafanya hayo kwakuwa wanafahamu kuwa, Uislamu unapotawala katika taifa lolote basi taifa hilo hujawa na irada ya kujitegemea na kamwe halikubali kuburuzwa. Vile vile ameashiria jinsi Wamagharibi wanashindwa kuficha furaha yao kutokana na baadhi ya matatizo ya kiuchumi yanayolikabili hivi sasa taifa la Iran na kusema, maadui hawachungi misingi ya kidiplomasia, kwani mwaka uliopita nchi mbalimbali za Ulaya zilishuhudia maandamano makubwa usiku na mchana na kwamba uchumi wa nchi hizo hizo za Magharibi uko katika hali mbaya zaidi huku zikikaribia kusammbaratika kabisa.
1117190
captcha