IQNA

Imam Khamenei: 'Viongozi Iran waongeze maradufu juhudi za maendeleo'

13:10 - October 18, 2012
Habari ID: 2433818
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amelitaka Baraza la Mawaziri la serikali ya Jamhuri ya Kiislamu, kuongeza juhudi maradufu katika kulitumikia taifa la Iran hadi kufikia kiwango kinachotakiwa.
Kiongozi Muadhamu ameyasema hayo Jumatano mwishoni mwa ziara yake ya siku nane mkoani Khorasan Kaskazini, wa kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kiislamu alipokutana na Baraza la Mawaziri la Iran na kusisitiza juu ya umuhimu wa kulitumikia vilivyo taifa sambamba na kutegemea tawfiqi ya Mwenyezi Mungu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kuwatumikia wananchi shupavu wa taifa hili, lazima kufikie kiwango cha juu cha ubora unaohitajika. Amesema, serikali inatakiwa kupitisha miswada kwa ajili ya maendeleo na uboreshaji wa hali ya mkoa wa Khorasan Kaskazini na kusisitiza kuwa, miswada yote lazima ifuatiliwe kwa umuhimu mkubwa. Akiashiria kwamba, mkoa wa Khorasan Kaskazini uko katika njia ya mamilioni ya wafanyaziara wanokwenda kumzuru Imam wa Nane, Imam Ridha (AS) amesema, kuna haja ya kuimarishwa sekta ya kilimo, sekta za utengenezaji wa bidhaa za vyakula viwandani na utalii. Wakati huo huo Muhammad Reza Rahimi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran pia ametoa ripoti kuhusu kazi zilizofanywa na zilizokusudiwa kufanywa na Serikali kwa minajili ya kutatua matatizo ya wananchi wa mkoa wa Khorasan Kaskazini na kuharakisha mwenendo wa maendeleo ya mkoa huo.
1120848
captcha