IQNA

Nyota wa soka barani Ulaya waitetea Palestina

12:55 - December 03, 2012
Habari ID: 2457793
Wachezaji soka kutoka ligi kubwa barani Ulaya wamekosoa vikali uamuzi wa Shirikisho la Soka Bara Ulaya (UEFA) wa kuandaa kombe la soka la ubingwa wa chini ya umri wa miaka 19 huko Israel mwakani.
Taarifa iliyotolewa na wachezaji hao imelaani hujuma ya hivi karibuni ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza na imetangaza mfungamano wa wacheza soka hao nyota na watu wa Ghaza ambao wanaishi katika mzingiro na wamenyimwa haki za kimsingi za binadamu na uhuru.
Eden Hazard wa timu ya Chelsea ya London, Yohan Cabaye wa Newcastle United na Abou Diaby wa Arsenal ni kati ya wachezaji kadhaa wa Ligi ya Primia ya England nchini Uingereza ambao wanaunga mkono kampeni hiyo na wamekosoa vikali hatua ya Israel kuendelea kuwashikilia bila kuwafunguliwa mashtaka wachezaji soka wawili Wapalestina.
Mapema mwaka huu nyota wa zamani wa Manchester United Eric Cantona aliwaandikia barua waandalizi wa mchuano huo na kusema: Kila siku Israel inatekeleza sera za ubaguzi, ukiukwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa sheria za kimataifa. Amesema kuwa kama ambavyo nchi za Ulaya zinashinikiza mataifa mengine yaheshimu haki za binadamu, zinapaswa pia kuishinikiza Israel iheshimu haki za Wapalestina.
Mkuu wa Shirikisho la Soka Palestina Jibril Rajoub pia amemwandikia barua mkuu wa UEFA Michel Platini akitaka mechi hizo zisichezwe Israel lakini Platini amekataa kutekeleza ombi hilo. 1146729

captcha