Akizungumza Jumanne katika kikao na waandishi habari, Ramin Mehmanparast ameashiria vitendo vya watu wenye kufurutu mipaka dhidi ya Waislamu wa Kishia Pakistan na kuongeza kuwa Iran inajitahidi kuepusha hitilafu za kimadhehebu na kikaumu. Amesema kuzusha hitilafu kama hizo ni katika njama dhidi ya Ulimwengu wa Kiislamu. Mehmanparast amesema wote wanapaswa kujitahidi kuzuia kuvunjwa umoja wa Waislamu.
Kuhusiana na kadhia ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar, Mehmanparast amesema Iran inafanya juhudi kuhakikisha wanatumiwa misaada ya kibinaadamu.
Mehmanparast pia ameitaka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kuchukua hatua za kivitendo kuzuia kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu.
Akijibu swali kuhusu kadhia ya nyuklia, Ramin Mehmanparast amesema 'Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA unapaswa kuweka wazi hatua ambazo Iran inapaswa kuchukua ili kuondoa wasiwasi kuhusu mpango wake wa nyuklia. Amesisitiza kuwa Iran inafungamana na majukumu yake katika fremu ya Mkataba wa Kuzuia Usambazwaji Silaha za Nyuklia NPT. Ameongeza kuwa shughuli za nyuklia za Iran zinafanyika kwa malengo ya amani.
1164577