IQNA

Imam Khamenei asisitiza kusimama kidete mbele ya maadui

13:58 - January 09, 2013
Habari ID: 2478092
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumanne asubuhi alionana na maelfu ya watu wanamapinduzi na wenye kushikamana na dini wa mjini Qum na kusisitiza kuhusu umuhimu wa taifa la Iran kusimama kidete mbele ya njama za maadui.
Ameongeza kuwa matunda yaliyojaa baraka na yalikuwa na matunda muhimu sana ya mapambano ya Dei 19 ya wananchi wa Qum yaliyodhihirisha wazi namna ahadi za Mwenyezi Mungu zinavyotimia na huku akisisitiza kuhusu wajibu wa kusimama kidete na kuwa macho kikamilifu katika kukabiliana na njama, mbinu na hila za maadui hususan wakati wa uchaguzi wa Rais wa mwezi Juni mwaka huu ametoa miongozo kadhaa kuhusu wajibu wa viongozi, watu maalumu na muhimu katika jamii na wananchi wote kwa ujumla, pamoja na vyombo vya habari na watu wenye nia ya kuwa wagombea katika uchaguzi huo.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amesisitiza kuwa ni jambo la dharura kuzingatia matukio ya kipindi cha Mapinduzi na ya miongo mitatu iliyopita na kupata funzo katika matukio tofauti yaliyobeba sifa ya kubakia milele katika historia kama vile tukio la Dei 19 na kuongeza kuwa, baadhi ya watu walikuwa wanasema wazi kuwa ni jambo lisiloyumkinika kabisa kwa taifa la Iran kuushinda utawala uliojaa ghururi na majigambo wa kitaghuti na kuulazimisha kuondoka katika Iran azizi jambo ambalo liliudhalilisha sana utawala wa kibeberu wa Marekani lakini kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, utawala wa kisultani na kifalme wa Iran umetupwa kwenye debe la taka za historia na sasa Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran limejikomboa kikamilifu mbele ya ubeberu wa Marekani na kupata heshima kubwa mbele ya walimwengu kiasi kwamba jina la taifa na utawala wa Kiislamu wa Iran linayafurahisha na kuyavutia mataifa mengine ya dunia (yanayopinga ubeberu na yanayopenda ukombozi).
Ameutaja ushindi wa kila namna na mafanikio makubwa liliyopata taifa la Iran katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita kuwa ni dhihirisho la kutimia ahadi za nusura ya Mwenyezi Mungu na huku akitoa ushahidi kutoka katika aya mbali mbali za Qur'ani Tukufu amesema: Mataifa ya waumini, yaliyo macho na yenye istikama, kwa yakini na bila ya shaka yoyote, wakati wake unapofika, hupata msaada wa Mwenyezi Mungu na kwamba uhakika huo ni sunna isiyobadilika ya Mwenyezi Mungu na ni kwa msingi wa sunna hiyo hiyo ya Mwenyezi Mungu ndio maana taifa la Iran limeweza kuwashinda maadui katika vipindi na hatua mbali mbali.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria udharura wa kuainsishwa kwa njia sahihi malengo na kutangazwa kwa njia bora misimamo sahihi ya taifa la Iran duniani na kuweko mipango makini ya kufanikisha malengo hayo na kuongeza kwamba: Kama taifa azizi la Iran, na vijana wenye moyo mzuri na wenye uwezo mkubwa wa Iran, litaendeleza njia yake hiyo kwa uimara wa hali ya juu, basi bila ya shaka yoyote sunna hiyo ya Mwenyezi Mungu inalijumuisha pia taifa hili kwa wakati unaofaa na kupelekea kufanikiwa malengo, matumaini na kaulimbiu zao zote za kitaifa, Kiislamu na kimataifa na kubadilisha kabisa mkondo wa historia na hivyo kuandaa mazingira ya kudhihiri Imam wa Zama, (Imam Mahdi AS), Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria jinsi wananchi wa Iran walivyo imara katika kukabiliana na njama za wa tawala za kibeberu zinazoshirikiana kuiwekea Iran vikwazo na kuongeza kuwa: Tofauti na huko nyuma, hivi sasa waistikbari wanakiri wazi wazi kuwa malengo ya vikwazo vyao ni kulichosha taifa la Iran, kuwachochea wananchi kukabiliana na mfumo wao wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu, kuongeza mashinikizo dhidi ya viongozi wa Iran na mwishowe kuwafanya wabadilishe misimamo yao.
Ameongeza kuwa: Amma msimamo wa wananchi wa nchi hii kubwa ni kushikamana na misingi ya Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu na kulinda heshima ya kitaifa ya Waislamu kadiri siku zinavyokwenda mbele na hilo kwa hakika ni jambo linalopingana kikamilifu na malengo ya maadui.
Vile vile ametoa ufafanuzi kuhusu sababu zinazoweza kusaidia sana katika kupambana na serikali za mabeberu na kuongeza kwamba, mwamko na kuwa macho taifa la Iran ni jambo la dharura sana.
Amesema: Inabidi sote kwa pamoja tujipambe kwa taqwa ya watu wote, tuwe macho na makini sote kwa umoja wetu mbele ya njama za adui na tusiruhusu jambo lolote lile litusahaulishe hatari za maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewausia na kuwasisitizia sana viongozi nchini, vyombo vya habari na mitandao ya Intaneti ijiepushe na kuwashughulisha watu na masuala ya pembeni na kuongeza kwa kusema kuwa: Anatoa nasaha zote hizo ili Wairani wawe macho wakati wote mbele ya adui, wasimsahau hata mara moja na watambue ni mpango na lengo gani hasa wanapaswa kulifuatilia.
Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia pia mantiki iliyotolewa yaani kuwa macho kitaifa kwa ajili ya kuelewa malengo na mipango ya adui na kuongeza kuwa, mtu unapovichunguza vitendo na maneno ya mabeberu utaona kuwa, hivi sasa akili ya adui imekita kwenye uchaguzi muhimu unaotarajiwa kufanyika nchini Iran miezi mitano ijayo yaani mwezi Khordad 1391 (Juni, 2013).
Aidha ametoa ufafanuzi kuhusu malengo, mbinu na njia zilizotumiwa na maadui katika uchaguzi wa 11 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, katika hatua yao ya kwanza na kama wataweza, basi maadui wanataka uchaguzi usifanyike kabisa nchini Iran lakini wanajua kuwa hilo hawaliwezi na ndio maana wamekata tamaa nalo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kuna wakati baadhi yao walijaribu kadiri walivyoweza kuhakikisha uchaguzi nchini Iran unaakhirishwa angalau kwa wiki mbili lakini sisi tulisisitiza kuwa uchaguzi hauwezi kuakhirishwa hata kwa siku moja na hivyo njia ya kuakhirisha uchaguzi ikafungwa kama ilivyofungwa kikamilifu njia ya kuzuia kabisa kufanyika uchaguzi.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kufanya njama za kuzuia wananchi wasishiriki kwa wingi katika uchaguzi kuwa ni lengo jingine la maadui linaloonekana wazi wazi na kuongeza kuwa, watu wote na hata wale watu ambao yumkini wakatoa nasaha kwa watu kutokana na kuumizwa na kuuonea uchungu uchaguzi wanapaswa kutambua vyema kwamba, hawapaswi kumsaidia adui katika jambo hilo.
Vile vile amewalaumu wale watu ambao mara kwa mara wamekuwa wakikariri maneno ya kufanyika kwa uhuru uchaguzi na kuongeza kuwa: Ni jambo lililo wazi kwa kila mtu kuwa inabidi uchaguzi ufanyike kwa uhuru. Kwani zaidi ya chaguzi 30 zilizofanyika nchini Iran katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, hazikuwa huru? Kuna nchi gani duniani inayoishinda Iran kwa kufanya uchaguzi kwa uhuru? Tahadharini, yasije maneno yenu hayo yakawakatisha tamaa wananchi kuhusiana na uchaguzi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea kubainisha mbinu zinazoweza kumsaidia adui kufikia malengo yake katika uchaguzi na kuhoji akisema: Ni katika nchi gani duniani ambapo hakuchujwi watu na hakuangaliwi watu gani wanastahiki kugombea? Kwa nini mnashikilia sana jambo hili ili kuwatwisha wananchi dhana kuwa hakuna faida ya kushiriki katika uchaguzi?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amewasisitizia wale watu ambao kwa kujua au kutokujua wanaendelea na njia hiyo akisema: Mungu apishie mbali msije mkakumbwa na mghafala na hivyo ikawa mnajaza jedwali iliyokusudiwa na adui.
Aidha amewalaumu wale watu ambao wanajaribu kuwabebesha watu wengine fikra kuwa uchaguzi si kitu cha lazima katika Uislamu na kuyataja madai na maneno kama hayo kuwa ni mbinu nyingine ambazo zinasaidia kufanikisha malengo ya maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Tab'an mimi pia ninasisitiza na kutilia mkazo suala la kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa wa salama na wenye uaminifu na kwamba viongozi wa serikali na wasio wa serikali wanatakiwa kuchunga na kuheshimu kikamilifu sheria, taqwa na usafi wa nafsi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa salama na kwa yakini hivyo ndivyo itakavyokuwa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia njia na mbinu nzuri sana zilizomo katika sheria za Iran kwa ajili ya kufanyika uchaguzi wa salama na kuongeza kuwa: Iwapo watu wote wataheshimu na kutekeleza vizuri sheria hizo, basi bila ya shaka yoyote uchaguzi utakuwa wa salama, ila labda watu watake kufanya mambo kinyume cha sheria kama ambavyo baadhi ya watu ambao hawakuheshimu sheria walivyosababisha fitna ya mwaka 2009 na kuwasababishia usumbufu wananchi na nchi, na kujisababishia wenyewe madhara makubwa sana na kuporomoka kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu njia ambazo zinaweza kumsaidia adui kufanikisha lengo lake kuu katika uchaguzi yaani kuwafanya wananchi wasusie uchaguzi na kuongeza kuwa: Yumkini baadhi ya watu wakajaribu kuwashughulisha wananchi na masuala mengine kwa kuzusha jambo fulani au kadhia fulani ya kiuchumi, kisiasa na kiusalama ambapo jambo hilo nalo ni katika mbinu za kuwasaidia maadui lakini mimi nina yakini kuwa wananchi wa Iran wana muono wa mbali sana na ni werevu mno kiasi kwamba hawawezi kulaghaiwa na mambo kama hayo ya kiuadui ya maadui na vibaraka wao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kuwazungumzia watu ambao wanatarajiwa kushiriki kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais nchini Iran katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka.
Amesema, kushiriki katika uchaguzi ni haki na ni jukumu na kuongeza kuwa: Kila mtu ambaye ana imani na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na anaikubali Katiba anataka kutumia haki yake hiyo au kutekeleza jukumu lake katika suala hilo na wako watu wengine ambao wanataka kuwathibitishia wananchi ustahiki wao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria jinsi ilivyo nzito kazi ya kuendesha nchi na kuongeza kuwa: Kazi ya uendeshaji wa nchi si ndogo, bali ni kazi nzito wanayobeba viongozi, hivyo watu wanaopaswa kuingia kwenye medani ya kugombea inabidi wao wenyewe wahisi ndani ya nafsi zao kuwa kazi hiyo wanaiweza.
Ameongeza kuwa: Yumkini kukawa kuna watu wanaofanya kazi katika daraja nyinginezo na ikawa baadhi yetu hatuwaoni. Jambo hilo amesema linaonesha ni kiasi gani kazi ya kuendesha nchi ni nzito, hivyo watu wanaojitokeza kugombea wanapaswa ndani ya nafsi zao wajue kuwa wanao uwezo wa kubeba jukumu hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Watu wanaojitokeza kuwania kiti cha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu kwa hakika wanapaswa kushikamana kikamilifu na mfumo unaotawala nchini na washikamane vilivyo pia na Katiba, na watake ndani ya dhati ya nafsi zao kwamba Katiba itekelezwe kwani Rais hula kiapo cha kuheshimu jambo hilo na mtu hawezi kula kiapo cha uongo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema mwishoni mwa hotuba yake kuwa: Inshaallah kwa uwezo na baraka za Mwenyezi Mungu, kutafanyika uchaguzi mzuri utakaowashirikisha watu wengi nchini Iran ifikapo mwezi Khordad 1392 (Hijria Shamsia sawa na mwezi Juni, 2013 Milaadia).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ametumia fursa hiyo ya hotuba yake mbele ya maelfu ya wananchi wa Qum kuwashukuru na kusifu nafasi muhimu sana ya wananchi wa mji huo katika matukio ya kabla na ya baada ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Kumbukumbu za harakati ya tarehe 19 Dei haipaswi kusahauliwa kwani kubainisha masuala hayo sambamba na kukifanya kizazi cha vijana kujua historia ya taifa lao hupelekea kutukuzwa na kuheshimiwa mchango wa jitihada kubwa za taifa hili na kuwafundisha vijana umuhimu wa kuwa macho na kusimama imara katika kukabiliana na maadui ambao kidhahiri wanaonekana wana nguvu na pia kuwafanya vijana watambue kuwa mwishowe ushindi utakuwa ni wao tu.
1168349
captcha