Mahakama ya Rufaa ya Bahrain Jumatatu hii ilitoa hukumu dhidi ya viongozi 13 wa upinzani ambao walikuwa wakituhumiwa kusababisha vurugu na machafuko. Mahakama hiyo ya rufaa imetangaza kuwa, hakuna ruhusa ya kukata rufaa kupinga hukumu hizo. Kwa mujibu wa hukumu hizo, viongozi 7 wa upinzani nchini Bahrain wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha jela, wanne kati yao wamepewa adhabu ya miaka 15 jela, huku wawili waliobakia wakihukumiwa miaka mitano jela. Viongozi hao wa upinzani wa Bahrain walitiwa mbaroni mwanzoni mwa vuguvugu la upinzani la wananchi wa nchi hiyo na kushtakiwa katika mahakama ya kijeshi.
Baada ya kushtadi wimbi la malalamiko ya kimataifa dhidi ya hukumu za mahakama ya kijeshi ya Bahrain, mwaka 2012 mafaili ya kesi za wanaharakati hao yakarejeshwa katika mahakama ya kiraia na mahakama hiyo ikaunga mkono hukumu za hapo awali zilizotolewa na mahakama ya kijeshi. Hata hivyo mawakili wa wanaharakati hao walikata rufaa na kesi hizo kusikilizwa katika Mahakama ya Rufaa na mahakama hiyo nayo kama ilivyokuwa kwa mahakama iliyotangulia, imeunga mkono hukumu hizo na hivyo kufunga kabisa mlango kusikilizwa tena kesi hiyo. Hukumu hiyo imekabiliwa na radiamali na malalamiko makubwa ya wapinzani nchini Bahrain. Wapinzani wa Bahrain sanjari na kulaani hukumu hiyo wametoa wito wa kukusanyika mbele ya jengo la Wizara ya Sheria mjini Manama. Wapinzani nchini Bahrain wanasema kuwa, mageuzi nchini humo yatapatikana tu kwa kuweko uadilifu na uhuru wa mahakama na kuongeza kwamba, hatua ya utawala wa Aal Khalifa wa nchi hiyo ya kuendesha siasa za ukandamizaji, utumiaji mabavu, sheria za kidhulma na mahakama zisizo na uhuru, lengo lake ni kubana uhuru wa wananchi na kufuatilia nyendo za wapinzani na wanaharakati wa kisiasa. Duru za karibu na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi zimefichua kwamba, utawala wa kifalme wa Bahrain umewaajiri maelfu ya wapiganaji wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq ambao wana uzoefu na tajiriba ya kukandamiza wapinzani ili waendeshe ukandamizaji dhidi ya wapinzani wa Bahrain.
Mamluki hao wamewasili Manama kwa ndege ya Gulf Air wakitokea Amman mji mkuu wa Jordan na akthari ya mamluki hao wameshaajiriwa katika kikosi cha ulinzi cha nchi hiyo na kupewa uraia. Wananchi wa Bahrain walianza harakati za kupinga serikali ya kifalme ya nchi hiyo mwezi Februari mwaka 2011 na serikali ya nchi hiyo imekuwa ikitumia njia tofauti kuzima harakati hiyo, ikiwemo ya kukandamiza maandamano na kuwatia mbaroni kiholela wanaharakati wa kisiasa. Ukweli wa mambo ni kuwa, ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Manama hadi sasa haujaweza kuzima sauti ya kutaka mageuzi ya wananchi wa Bahrain inayoendelea kusikika katika anga ya nchi hiyo.
1169170