Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo Jumatano alipokutana na maafisa na wafanyakazi wa Idara ya Usalama katika Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Huku akiashiria jinsi ahadi za Mwenyezi Mungu zinavyotimia bila ya shaka wala wasiwasi wowote kwa watu wanaosubiri, wanaotawakali Kwake na wanaoihami na kuinusuru dini Yake, Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa: Ushahidi wa wazi wa kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu ni mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao licha ya kuweko mashinikizo na njama zote hizi za maadui lakini hivi sasa na baada ya kupita miaka 34 ya tangu kuasisiwa kwake umekuwa ni mfumo wenye kuheshimika, wenye nguvu na wenye taathira katika masuala ya kieneo na kimataifa na ni mfumo wenye taifa kubwa lenye welewa mpana, linalomtambua vizuri adui na kuzielewa vyema nyakati na lenye maendeleo makubwa ya kielimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha sambamba na kusisitiza kuwa kuna wajibu wa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu wakati wote na kuwa na nia nzuri na matumaini mema kuhusu kupata msaada wa Mwenyezi Mungu ameongeza kuwa: Kambi ya uistikbari imefanya juhudi zake zote na kutumia nguvu zake zote ili kulilazimisha taifa la Iran lisalimu amri kupitia vikwazo na mashinikizo yake lakini taifa hili limeamua kuvumilia tabu kwani limeshazijua njama na hila za adui pamoja na malengo, shabaha na stratijia zake na kwamba taifa hili linafanya mambo yake kulingana na welewa na utambuzi wake sahihi kuhusu adui yake.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa, kama ambavyo ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ulipatikana mwaka 1979 katika mazingira yasiyotarajiwa na hivyo kuwa ushahidi wa wazi wa kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu, ni vivyo hivyo kuendelea kuwepo Mapinduzi ya Kiislamu na kuzidi nguvu zake, uwezo wake na maendeleo yake ya kila upande, tena licha ya kuweko pepo nyingi kali na mashinikizo makubwa na mazito ya adui na ya ulimwengu wa kibeberu, nao ni ushahidi mwingine wa wazi wa kutimia kivitendo ahadi za Mwenyezi Mungu.
Vile vile ameitaja sifa ya wananchi wa Iran ya kuwa na ufahamu, welewa, kumtambua adui na kuzijua vizuri nyakati kuwa ni jambo la ajabu na kuongeza kuwa: Katika matukio ya mwaka 2009 ambapo adui alidhani kuwa amefanikiwa kufanikisha njama zake za miaka 10 dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wananchi wa Iran walijitokeza kwa nguvu kubwa katika medani na kutoa pigo kubwa kwa wapinzani na maadui wa kimataifa, hatusemi tena vitimbakwiri na vibaraka wao wa ndani ambao hawana nafasi yoyote mbele ya adhama ya taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Taifa la Iran kwa mara nyingine litawadhihirishia waliwengu nguvu, uimara, ufahamu na welewa wake mpana wa mambo katika siku ya maadhimisho ya Bahman 22 (Februari 11, siku zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran).
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesema katika sehemu nyingine ya hotuba yake kuwa ni jambo la fakhari na lenye heshima na umuhimu kubwa kulinda usalama na kudhamini amani ya vikosi vya ulinzi na kuongeza kuwa: Kwa mtazamo wa Uislamu vikosi vya ulinzi si majimui ya kimakanika na wala si kama gari isiyo na udhibiti wowote, bali vikosi vya ulinzi kwa mujibu wa Uislamu ni taasisi ya mwanadamu yenye majimui ya watu wenye akili na busara, azma, nia ya kweli na msimamo thabiti na yenye imani na hisia.
1172963