Akizungumza alipotembelea Kituo Cha utamaduni Cha Iran mjini Tunis, Sheikh Musa amesema kuweko madhehebu katika Uislamu si tatizo kwani Waislamu wote kwa pamoja wana itikadi moja kuhusu Tauhid, Qur'ani na Mtume Muhammad SAW. Amesema hitilafu chache za kifiqhi si jambo la kuzuia umoja halisi baina ya Waislamu Mashia na Masunni.
Sheikh Abdul Latif Musa, ambaye aliwahi kufukuzwa Tunisia wakati wa utawala wa dikteta aliyeangusha Ben Ali, amesifu msimamo imara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya madola ya kibeberu duniani. Aidha amesema sera ya Iran ya kutafuta Umoja wa Kiislamu inaenda sambamba na Sirah ya Mtume SAW.
Mwanazuoni huyo wa Tunisia ametoa wito kwa Waislamu kote duniani kutambua umuhimu wa umoja na kukabiliana na njama za maadui wa Uislamu.
"Daima nimekuwa nikisisitiza katika hotuba zangu za sala ya Ijumaa kuwa tuhuma dhidi ya Iran hazina msingi." Mwanazuoni huyo wa Tunisia amehoji, " Ni vipi baadhi ya Waislamu wanaituhumu Iran katika hali ambayo Iran imesimam kidete kuwatetea Waislamu wanaodhulumiwa huko Palestina? "
Katika mkutano huo mkuu wa Idara ya Utamaduni ya Iran mjini Tunis Bw. Sadiq Ramadhan amesisitiza umuhimu wa umoja wa Waislamu. Aidha amemkabidhi Sheikh Abdul Latif Musa zawadi ya Qur'ani Tukufu iliyochapishwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
1172351