Ali Larijani amesema kuwa nchi za Kiislamu zinapaswa kuyatazama mambo kwa uangalifu na kuchukua hatua kwa maslahi ya umma wa Kiislamu kwa kuzingatia hali nyeti ya mambo ya sasa katika eneo. Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo jana jioni katika ufungaji wa kikao cha nane cha Kimataifa cha Mabunge ya Nchi za Kiislamu huko Khartoum mji mkuu wa Sudan. Larijani amesema anatumai kuwa mazingira yataandaliwa kwa ajili ya kuimarisha umoja na ushirikiano wa nchi za Kiislamu kutokana na kuwa kikao hicho cha Khartoumm kimefanyika lengo likiwa ni kuzikurubisha pamoja nchi hizo.
Jumuiya ya Mabunge ya Kiislamu ilianzishwa kwa pendekezo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa sasa ina nchi wanachama 53.
Kwa sasa Jumuiya ya Mabunge ya Kiislamu inaonekana kuwa na umuhimu mkubwa zaidi katika kipindi hiki ambapo mataifa ya Kiislamu yameamka chini ya kivuli cha harakati ya mwamko wa Kiislamu inayoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali duniani.
Kwa sasa madola ya kibeberu yameanzisha mikakati mipya baada ya kufeli mbinu za Marekani na waitifaki wake huko Afghanistan, Iraq na Lebanon. Madola hayo sasa yanafanya jitihada kubwa kuhakikisha kwamba maslahi yao ya kikoloni yanaendelea kulindwa katika nchi zilizofanya mapinduzi dhidi ya tawala tegemezi na vibaraka kama Tunisa, Misri, Libya Yemen na kadhalika.
Kwa msingi huo inatarajiwa kuwa mabunge ya Kiislamu yatakuwa na nafasi kubwa katika kuongoza mapinduzi ya wananchi dhidi ya tawala za kidikteta na kubadilishana mawazo kuhusu masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu.
1176697