Kiongozi Muadhamu ameyasema hayo leo asubuhi mjini Tehran alipohutubia Baraza la Mawlid kwa mnasaba wa kukumbuka kuzaliwa Mtume Muhammad SAW na mjukuu wake Imam Ja’afar Sadiq AS. Kikao hicho kimehudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu wa mfumo wa Kiislamu, wananchi wa matabaka mbali mbali, washiriki wa Kongamano la 26 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu pamoja na mabalozi wa nchi za Kiislamu. Katika hotuba yake Kongozi Muadhamu amesema sera kuu za madola ya istikbari ni kukabiliana na mwamko wa Kiislamu na kuwagonganisha Waislamu katika nchi za Kiislamu. Ameashiria pia mwamko katika ulimwengu wa Kiislamu hasa kaskazini mwa Afrika na kusema mwamko huo ni sehemu ya kutimia ahadi ya Allah SWT. Kiongozi Muadhamu amesema kwa kuzingatia njama za maadui dhidi ya mwamko wa Kiislamu, viongozi wa kidini, kisiasa na wasomi wa vyuo vikuu katika Ulimwengu wa Kiislamu wanapaswa kuandaa mikakati imara ya kukabiliana na maadui wa Umma wa Kiislamu na kuchukua hatua madhubuti za kutekeleza kivitendo nara ya Umoja wa Kiislamu. Kiongozi Muadhamu amesema kupitia Mwamko wa Kiislamu, Ulimwengu wa Kiislamu sasa uko tayari kutekeleza kivitendo maamurisho ya Bwana Mtume SAW. Amesema baada ya miongo kadhaa ya mashinikizo na ubeberu wa Wamagharibi katika Ulimwengu wa Kiislamu, hivi sasa Waislamu wanahisi kuwa ni Uislamu pekee ndio unaoweza kuwapatia izza, heshima na uhuru kamili. Amesema malengo makuu ya Ummah wa Kislamu yanaweza kufikiwa kwa baraka za Uislamu. Ayatulahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema nara ya ‘Umoja wa Kiislamu’ ni nara takatifu na kuongeza kuwa, Imam Khomeini MA Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote cha maisha yake alisisitiza kuwa anaamini udugu wa Kiislamu na kwamba mkondo huu umeendelea baada yake hadi leo. Kiongozi Muadhamu amesema njia pekee ya kukabiliana na njama za maadui ni kuwepo umoja miongoni mwa Waislamu. Ametoa mifano hai ya kuibuliwa hitilafu baina ya Waislamu na kutaja maafa ya Pakistan, vita na mauaji Syria, kususiwa sauti ya watu wa Bahrain na kuwagonganisha watu wa Misri. Kiongozi Muadhamu amesema, ‘kwa yakini harakati za kuibua hitilafu miongoni mwa Waislamu zimepangwa na maadui.’
1179826