IQNA

'Mapinduzi ya Kiislamu ni zawadi kutoka kwa Allah'

19:26 - February 08, 2013
Habari ID: 2493316
Ayatullah Muhammad Ali Mowahedi Kermani Khatibu wa sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo mjini Tehran amesema kuwa, ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ulioongozwa na Imam Khomeini MA, ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo imewapa wananchi wa Iran izza na utukufu na kuwaepusha na vitendo vya dhulma, ukandamizaji na ukoloni.
Ameongeza kuwa ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu ya Iran unatokana na ahadi ya Mwenyezi Mungu ya haki kushinda batili, ameongeza kuwa, iwapo madola yote ya kibeberu yatasimama kidete dhidi ya haki, kwa idhini ya Allah, haki itayasambaratisha madola yote ya kibeberu. Ayatullah Kermani ameongeza kuwa, malengo ya madola ya Magharibi ya kuiwekea vikwazo na mashinikizo taifa na wananchi wa Iran, ni kutaka wananchi wa Iran wavunjike moyo na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Akihutubia halaiki kubwa ya waumini katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini MA, Ayatullah Kermani amezitaja njama za hivi karibuni za madola ya kibeberu na uzayuni duniani za kuzusha mifarakano kati ya mataifa ya Kiislamu na hasa hitilafu baina ya Mashia na Masuni katika baadhi ya nchi, na kuongeza kuwa, iwapo nchi za Kiislamu zitashikilia umoja na mshikamano wao, hakuna dola lolote litakaloweza kuwashinda. Ayatullah Kermani amewausia maulama, wanazuoni na viongozi wa nchi za Kiislamu kuzuia kujipenyeza siasa za kuzusha hitilafu za madola ya kibeberu na Wazayuni na kuwataka wawe macho katika kuzima njama hizo zilizo dhidi ya Uislamu. Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Kermani ameisifu misimamo ya siasa za kigeni ya Iran kuhusiana na mgogoro wa Syria na kusema kuwa, kushindwa magaidi nchini Syria kumefuta kabisa malengo machafu ya Marekani, baadhi ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati na utawala wa Israel za kuisambaratisha serikali ya Syria, na kwamba hivi sasa Marekani inafikiria suala la kufadhilisha njia ya mazungumzo katika kutatua mgogoro unaoendelea kutokota nchini humo.
1185283
captcha