IQNA

Katibu Mkuu wa Hizbullah aionya vikali Israel

20:47 - February 17, 2013
Habari ID: 2498006
Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrallah amesema harakati ya mapambano au muqawama Lebanon iko tayari kuilinda nchi hiyo endapo utawala haramu wa Israel utathubutu kutekeleza hujuma dhidi yake.
Akizungumza Jumamosi mjini Beirut katika hafla ya kuwaenzi mashahidi wa Hizbullah, Sayyid Nasrallah amewaonya Waisraeli kuwa harakati ya mapambano haitanyamazia kimya hujuma yoyote.
Sayyid Nasrallah amekanusha uvumi kuwa Hizbullah imedhoofika na kuongeza kuwa harakati ya mapambano iko tayari zaidi ya wakati wowote ule. Kwingineko katika matamshi yake, katibu mkuu wa Hizbullah amesema mapambano ndio chaguo pekee la Wapalestina katika kukabiliana na utawala ghasibu wa Israel. Ameongeza kuwa, 'Israel ndio tishio kubwa zaidi kwa Palestina na eneo.' Sayyid Nasrallah amesema Hezbollah itaendelea kuwaunga mkono Wapalestina ili wapate haki zao.
Bila shaka kusimama kidete wananchi wa Lebanon dhidi ya Wazayuni kwa uongozi wa Harakati ya Hizbullah kumejenga ngome imara dhidi ya uchokozi wa utawala wa Kizayuni. Suala linalopaswa kukumbushwa hapa ni kuwa, kila siku maqawama unazidi kupendwa na wananchi wa Lebanon na fikra za waliowengi katika eneo huku suala hilo likipewa kipaumbele na viongozi wa nchi hiyo. Harakati ya muqawama nchini Lebanon iliyopelekea kushindwa mara kadhaa utawala wa Kizayuni katika miaka kadha iliyopita, inabainisha mabadiliko ya uwiano yaliyoshuhudiwa kutoka upande wa viongozi wa Tel Aviv na washirika wao katika eneo. Israel na washirika wake kwa kuendeleza siasa za kuzusha wasiwasi na woga katika eneo na kuongopa kwamba utawala huo hauwezi kushindwa, wamekuwa wakikusudia kuangamiza muqawama mkabala na kujipanua utawala huo na madola ya kibeberu katika Mashariki ya Kati. Lakini kushindwa utawala huo kutokana na kusimama kidete wananchi wa Lebanon, ambako kulishuhudiwa wazi mwaka 2000 Miladia, kumekwamisha mipango na njama za Israel na Marekani dhidi ya Lebanon na eneo zima kwa ujumla.
Kushindwa huko kulipelea Israel irudi nyuma kutoka katika maeneo ya Lebanon iliyokuwa ikiyakalia kwa mabavu mwaka 2000. Kushindwa Tel Aviv na muqawama kuliendelea kushuhudiwa katika vita vya siku 33 mwaka 2006 na hivyo kuvunja kabisa madai ya uongo ya kutoshindwa utawala huo katika medani ya vita. Hii ni katika hali ambayo, kushindwa Israel katika vita hivyo, kulikwamisha kabisa mpango wa kibeberu wa Marekani kwa ajili ya Masahariki ya Kati uliojulikama kama 'Mashariki ya Kati Mpya' uliokuwa ukifuatiliwa kwenye vita hivyo. Muqawama wa Lebanon umebadilika na kuwa kigezo cha mapambano ya mataifa ya eneo dhidi ya utawala wa Kizayuni, na ushindi wake umeongeza nguvu na matumaini kwa Wapalesina katika mapambanao yao dhidi ya adui Mzayuni. Uzoefu unaonesha kuwa, kusimama kidete na kuendeleza muqawama ndiyo njia pekee ya kukabiliana na siasa za kupenda kujitanua za Israel, kwani njia za suluhu hazijakuwa na faida yoyote zaidi ya kushadidisha siasa za kupenda kujitanua na jinai za utawala huo. Hii ndio sababu Sayyid Hassan Nasrullah sambamba na kubainisha wazi kuwa aduia mkuu wa wananchi wa eneo la Mashariki ya Kati ni Israel na washirika wake, akasisitiza udharura wa kudumishwa muqawama na kusimama kidete dhidi ya Wazayuni.
1189627
captcha