IQNA

Imam Khamenei: Kadhia ya Palestina ni muhimu katika utengenezaji filamu

16:00 - February 21, 2013
Habari ID: 2500260
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, Kujihami Kutakatifu, Palestina na Mwamko wa Kiislamu ni kati ya maudhui ambazo ni muhimu zitumike katika utengenezaji filamu.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo Jumanne alipoonana na majimui ya wakuu na maafisa wa Tamasha la Wananchi la Filamu ya Ammar. Katika muongozo wake amelitaja suala la kuzingatiwa dini na mafundisho ya kidini pamoja na Mapinduzi ya Kiislamu na matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu katika tamasha hilo kuwa ni hatua nzuri sana na kusisitiza kuwa, mtazamo wa sanaa ya Kiislamu na tasnia ya filamu za kidini inabidi uwe wa muda mrefu unaokwenda sambamba na mipango makini na yenye kuleta matumaini ya mustakbali bora sambamba na kutumia vizuri zana ya sana kwa ajili ya kutoa taathira kubwa kadiri inavyowezekana.
Vile vile ameelezea kufurahishwa kwake na kufanyika tamasha hilo la wananchi la filamu ya Ammar na kusema kuwa, kuteuliwa jina la Ammar ambaye ni miongoni mwa masahaba wakubwa wa Bwana Mtume Muhammad SAW na pia miongoni mwa wafuasi wa karibu wa Imam Ali AS ni uteuzi mzuri sana na huku akiashiria sifa maalumu na za aina ya kipekee za sahaba huyo mkubwa wa Mtume Muhammad SAW ameongeza kuwa: Sifa ya kutotetereka aliyokuwa nayo Ammar katika matukio tofauti ya mwanzoni mwa Uislamu na vile vile mitihani mikubwa iliyomkumba baada ya kufariki dunia Mtume Muhammad SAW ikiwa ni pamoja na sifa yake ya kutambua vizuri zama na nyakati na kuchukua hatua zinazofaa na kwa wakati unaofaa na kubainisha waziwazi matukio yalivyokuwa katika kipindi cha Imam Ali AS ni miongoni mwa sifa maalumu alizokuwa nazo Sahaba Ammar (bin Yasir).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema kwamba, kuwa na mtazamo wenye matumaini na mustakbali mzuri na kupandisha juu kiwango cha mtazamo wa watu chini ya kivuli cha malengo makuu na matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu ni jambo muhimu sana na kusisitiza kuwa: Harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo ushindi wake ulianza mwaka 1979 na kuvunjwa haiba na nguvu za Marekani katika matukio tofauti kwenye kipindi chote hiki cha miaka 34 ya tangu kupatikana ushindi huo, yote hayo ni utangulizi wa kufikia kwenye malengo makuu ya mfumo wa Kiislamu, hivyo inabidi kuna wajibu wa kuongeza kasi zaidi kuelekea kwenye vilele vya juu vya mafanikio kwa hima na idili kubwa zaidi na kutomuogopa adui na njama zake na kujiepusha na kuangalia mambo kwa jicho baya na kuvunjana moyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema pia kuwa ni jambo la dharura kuwa na mtazamo huo katika masuala ya sana ya Kiislamu na tasnia ya filamu za kidini na kusisitiza kuwa: Vijana waliopambika kwa sifa bora za imani, wenye vipaji, shauku, mitazamo mipya na hima kubwa, ni injini ya kusukuma mbele gurudumu la harakati hiyo na kwamba watu wenye uzoefu katika kazi hiyo nao wanapaswa kutumia tajiriba na uzoefu wao, kulea nguvu kazi mpya na bora itakayoweza kuongeza kasi ya mwendo wa gurudumu hili.
Vile vile ameashiria msingi wa Kimagharibi wa sanaa ya sinema na udharura wa kuwa na mipangilio mizuri na kuundwa timu maalumu ya wanafikra kwa ajili ya kuongoza vizuri harakati za vijana na vipaji vipya kuelekea kwenye sana ya Kiislamu na tasnia ya filamu za kidini na vile vile kuingia watu walioshikamana na dini na matukufu ya Mapindizu ya Kiislamu na wenye utaalamu na uzoefu, katika sanaa hiyo muhimu.
Wakati huo huo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja sharti kuu la kuingia watu wa dini na wanamapinduzi na kuweza kutoa athari nzuri katika sanaa ya filamu, ni kujiwekea kinga kwa kuchunga ipasavyo mafundisho ya dini. Amefafanua jambo hilo akisema: Njia pekee ya kujiwekea kinga ni kuwa na uhusiano wa kuendelea na wa karibu na Mwenyezi Mungu, kutekeleza ibada za suna na kunyenyekea mbele ya Mwenyezi Mungu kama ambavyo Ammar aliweza kujipamba kwa sifa hizo na hivyo kupata kinga ya kutokumbwa na maradhi ya kutetereka.
Ameongeza kuwa: Ibada na dhikri na kumzingatia Mwenyezi Mungu ni kitu kitamu na chenye ladha nzuri kabisa kuliko sanaa yoyote ile.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja nafasi ya wakuu wa masuala ya sanaa na vituo vya Vyuo Vikuu vyenye taathira katika anga ya sinema na vyombo vya habari nchini kuwa ni muhimu na kusisitiza kuwa: Ili kuweza kuleta marekebisho katika jambo hilo, kunahitajika kufanyika marekebisho ya kimisingi ya kuingilia kwenye tasnia hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Watu ambao leo hii wanajishughulisha na kazi za filamu zenye maudhui za Mapinduzi ya Kiislamu na vita vya kujihami kutakatifu, kwa hakika wamo katika jihadi.
Aidha amesema, kutumia vizuri zana ya sanaa na kustafidi vyema na visa, hadithi na filamu zilizoandikwa vizuri kuwa ni miongoni mwa mambo ya dharura na ya kimsingi katika utengenezaji wa filamu na kusisitiza kuwa: Suala la uandishi wa hadithi na riwaya nchini bado uko mbali sana na nukta inayokusudiwa kufikiwa nchini na inabidi kitengo hicho nacho kitiwe nguvu zaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja baadhi ya maudhui kama zile zinazohusiana na historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, vita vya kujihami kutakatifu, Palestina na suala zima la mwamko wa Kiislamu kuwa ni miongoni mwa maudhui muhimu na zenye mambo mengi sana ya kutengenezewa filamu na kuongeza kuwa: Moja ya mambo ya uongo yanayopigiwa propaganda duniani leo ni pale wanaopiga propaganda hizo wanapodai kuwa sanaa haipaswi kuchanganywa na masuala ya siasa wakati ambapo kiwango kikubwa cha sanaa za Holly Wood kimejaa masuala ya siasa na kama si hivyo kwa nini basi filamu za Iran zinazopinga Uzayuni hazipewi ruhusa ya kushiriki kwenye matamasha ya filamu ya Holly Wood?
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Kutengeneza filamu za kisiasa zilizo dhidi ya Iran au kuzipa zawadi filamu zilizo dhidi ya Iran ni mambo yanayoonesha wazi kuwa sanaa ya Marekani na Magharibi imejaa masuala ya siasa.
Vile vile katika kikao hicho ameashiria suala la uhusiano wa elimu ya Sayansi ya Jamii (Humanities) na sanaa na sinema na wajibu wa kufanyiwa mapinduzi elimu ya Sayansi ya Jamii nchini akiongeza kuwa: Sayansi ya Jamii ni sawa na hewa anayoihitajia mwanadamu kuweza kupumua na kuvuta pumzi kwa majimui za watu muhimu na wenye vipawa ambao wana jukumu la kuiongoza jamii nchini hivyo suala la usafi na uchafu wa hewa hiyo ni muhimu mno kwa jamii.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja tatizo la Sayansi ya Jamii ya Magharibi kwamba ni kutokana na kuwa imesimama juu ya misingi ghalati ya maarifa na kusisitiza kuwa: Kuleta marekebisho katika elimu ya Sayansi ya Jamii na mapinduzi katika sinema na televisheni bila ya kurekebisha misingi ya maarifa ya Sayansi ya Jamii ya Magharibi ni jambo lisilowezekana kabisa; na kurekebisha msingi huo nako kunafungamana kikamilifu na kuwa na uhusiano mkubwa na vyuo vya kidini na maulamaa wa kidini.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaka mirengo yote ya sinema yenye mielekeo ya kidini na kimapinduzi ijiepushe na masuala ya pembeni wala kushughulishwa na hitilafu zisizo na maana.
Ameongeza kuwa: Watu wenye imani ya dini na wanamapinduzi yumkini wakawa na mitazamo yao tofauti katika masuala ya sinema lakini wanachopaswa kufanya ni kuweka pembeni mitazamo yao binafsi na kutia hima na juhudi zaidi kwenye masuala makuu na ya kimsingi.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, mabwana Vahid Jalili, Nader Talibzade, Hasan Abbasi, Mahdi Naseri, Sayyid Jamal Uud Simin, Abul Qasim Talebi, Farajullah Salahshour, Muhammad Sadiq Bateni, Ibrahim Fayyadh, Said Qasemi na Mustafa Rezvani walizungumza wakiwa ni majaji na washindi katika Tamasha la Filamu la Ammar na kujadili nukta zifuatazo:
- Udharura wa kuifanya sanaa kuwa ya watu wote hususan katika vitengo vya sinema kuanzia hatua ya uzalishaji hadi wakati wa uoneshaji na kuitoa katika anga ya hati miliki.
- Kutia nguvu na kuamilisha uwezo uliosahauliwa wa sanaa kwa ajili ya kutumikia malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu.
- Udharura wa kustafidi vizuri na vyombo vya sinema kwa ajili ya kufikisha sauti na daghadagha za kidini na kimapinduzi.
- Ulazima wa kutiwa nguvu sauti ya kiitikadi ya utengenezaji filamu za kidini kwa ajili ya kujiwekea kinga ya kutoathiriwa vibaya.
- Udharura wa kuwa na nguvu za kusema kwa ajili ya sinema na vyombo vya habari katika kuweka siasa na mipango mikuu ya nchi.
- Kujiepusha na kuwa na mtazamo wa udunishaji mambo katika teknolojia ya sinema na mipango mingineyo kwa ajili ya harakati za kimaendeleo.
- Kuweka mipango mizuri kwa ajili ya nguvu kazi mpya na kuwa na vigezo vizuri vya kufuata katika masuala ya tasnia ya sinema.
1191770
captcha