aarifa iliyotolewa leo na jeshi hilo imesema, kuanzia juzi Jumamosi wapiganaji 14 wa Boko Haram wameuawa na wengine 20 wamekamatwa, huku jeshi nalo likipoteza askari wake watatu.
Baadhi ya duru zimeripoti kuwa, raia wengi katika maeneo yanakofanyika opereseheni za jeshi la Nigeria dhidi ya wafuasi wa Boko Haram wamekimbia makazi yao na kutafuta hifadhi katika nchi za Cameroon na Niger. Mashambulizi makubwa ya vikosi vya jeshi la Nigeria yalianza Jumanne iliyopita, baada ya Rais Goodluck Jonathan kutangaza hali ya hatari katika mikoa mitatu ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, inakohesabiwa kuwa ngome muhimu zaidi ya wafuasi wa Boko Haram.
Ndege za kivita na helikopta zenye mizinga zimetumika kushambulia kambi za mafunzo za Boko Haram. Imearifiwa kuwa waasi hao wamelenga ndege moja kwa makombora ya kutungua ndege lakini hawakufanikiwa kuiangisha huku kituo chao kikiharibiwa kabisa. Karibu watu 3,500 wamepoteza maisha Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009. Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila.
Umasikini kwa upande mmoja na upendeleo mkubwa baina ya Wakristo na Waislamu nchini Nigeria kwa upande wa pili ni moja ya sababu zinazotajwa na wataalamu wa mambo kuwa chanzo cha vijana wa nchi hiyo kujiunga na kundi la Boko Haram. Licha ya Nigeria kupata pato kubwa kutokana na kuuza mafuta, asilimia 70 ya wananchi wa nchi hiyo wanaishi chini ya mstari wa umasikini. Hii ni katika hali ambayo, hali ya maisha ya Wakristo nchini Nigeria ni bora zaidi ikilinganishwa na ya Waislamu; na Wakristo wamekuwa wakinufaika zaidi na pato la mafuta ya nchi hiyo kuliko Waislamu.
1230537