Khatibu wa sala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo mjini Tehran amesema kuwa, kujitokeza kwa wingi wananchi wa Iran kwenye duru ya 11 ya uchaguzi wa rais hapa nchini, kutaulinda mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu katika kukabiliana na njama za maadui.
Ayatullah Muhammad Ali Movahhedi Kermani ametoa mkono wa pongezi kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Ali AS na kusema kuwa, kujitokeza kwa wingi wananchi wa Iran katika uchaguzi wa rais utakaofanyika Juni 14 ni hamasa kubwa itakayolinda mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ayatullah Kermani ametaja sifa maalumu anazopaswa kuwa nazo rais atakayechaguliwa na wananchi kuwa awe mcha Mungu, mwenye hekima, tadbiri, kiongozi, mwenye ufanisi na mwadilifu pamoja na kuzingatia kuwatumia watu mahiri na wachapakazi kwenye serikali yake. Khatibu wa sala ya Ijumaa mjini Tehran amesema kuwa, rais wa nchi anapasa kuwa mtu mwenye kutii na kufuata miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuwahudumia wananchi bila upendeleo. Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Kermani amekumbushia tukio la kukombolewa mji wa Khorramshahr uliokuwa umetekwa na utawala wa baath wa Iraq na kusisitiza kuwa, kumwamini Mwenyezi Mungu, subira na ushujaa wa wananchi wa Iran, ndio siri ya ushindi na kukombolewa mji huo.
1232850