Aliyasema hayo Ijumaa ya tarehe 27 Rajab iliyosadifiana na maadhimisho ya siku ya kubaathiwa na kupewa Utume Mtume wetu Muhammad SAW. Kwa mnasaba huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei ameonana na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na wawakilishi na mabalozi wa nchi za Kiislamu waliopo nchini Iran na majimui ya familia za mashahidi.
Ayatullah Udhma Khamenei sambamba na kutoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kupewa Utume Mtume Muhammad SAW amelitaja jukumu muhimu na kubwa zaidi la umma wa Kiislamu katika mazingira yalivyo hivi sasa duniani ni kuwa macho na kutambua vizuri ramani ya njia na pia kuzielewa vizuri njama za maadui wa Uislamu.
Ameongeza kuwa: Njama kuu za adui zimejikita kwenye kuleta hitilafu na mizozo kati ya Waislamu hivyo jambo lililo muhimu zaidi na la dharura zaidi hivi sasa ni umoja, mshikamano na ushirikiano kati ya Waislamu.
Vile vile ameashiria bugdha na chuki za maadui wa Uislamu kwa mwito wa haki wa mtukufu huo na jinsi chuki hizo zinavyoshuhudiwa mara kwa mara na kuongeza kuwa: Upinzani wa maadui hao kuhusu mlingano wa haki wa Mtume Muhammad SAW siku zote ulikuwa ni mkubwa sana na ulikuwa wa pande zote na uliendelea kuwepo kwa sura tofauti hadi mwisho wa umri uliojaa baraka wa mtukufu huyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, leo hii pia kuna upinzani mkubwa wa adui dhidi ya mwito wa Uislamu na kuongeza kuwa: Baada ya aidiliojia zisizo za Kimwenyezi Mungu kama vile aidiliojia ya Kimaksi na Kiliberali kushindwa kumletea ufanisi na utatuzi wa matatizo yake mwanadamu, leo hii nyoyo na macho ya walimwengu yameelekea upande wa Uislamu, na ni kwa sababu hiyo ndio maana hivi sasa uadui dhidi ya Uislamu ambao ni dini yenye aidiolojia bora kabisa ya uadilifu, heshima na utukufu wa mwanadamu, ukawa mkubwa sana.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amekitaja kitendo cha maadui wa Uislamu cha kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW kuwa ni moja ya mifano ya uadui huo mkubwa dhidi ya dini hii tukufu ya Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa, haiwezekani kuamini kwamba kitendo cha kuvunjiwa heshima Uislamu na kuenezwa chuki dhidi ya dini hii ya Mwenyezi Mungu kinafanyika bila ya mipango maalumu ya mashirika ya kijasusi ya madola ya kibeberu na uungaji mkono wao wa kifedha kwa jambo hilo.
Aidha amesititiza kuwa, baadhi ya vitendo vinavyofwanya na Waislamu kama vile kuwa na fikra mgando, kutokubali mabadiliko na kutowavumilia wengine vinatumiwa na madola ya kibeberu kama kisingizio cha kueneza uadui na propaganda mbaya dhidi ya Uislamu na kuongeza kuwa, Waislamu wana jukumu la kuutangaza Uislamu wazi wazi, kwa ushujaa, ukweli na uadilifu ili kwa njia hiyo waweze kuzivutia nyoyo za watu upande wa mafundisho matukufu ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Waislamu wanapaswa kusimama kidete kukabiliana na uadui wa maadui wa ujumbe wa Uislamu kama ambavyo Bwana Mtume Muhammad na Waislamu wengine wa huko nyuma walivyosimama kidete kuitetea dini hii ya Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuwa na tabasuri na muono wa mbali umma wa Kiislamu pamoja na Waislamu kujua ramani yao ya njia na njama za adui yao, kuwa ni jambo lenye udharura mkubwa na kuongeza kwamba: Njama kuu za adui ni kuzusha hitilafu kati ya Waislamu na kukuza taasubu za kimadhebu ili kuwagombanisha na kuwazozanisha Waislamu wenyewe kwa wenyewe ili kwa njia hiyo waweze kuupotosha umma wa Kiislamu na kuufanya usishughulishwe na adui yao mkuu yaani mabepari mafisadi na Wazayuni maghasibu wasio na chembe ya huruma.
Aidha amesisitiza kuwa: Umma mzima wa Kiislamu, iwe ni wanasiasa, wasomi na wengineo, wanapaswa waijue vizuri ramani hiyo ya njia ya adui ili kwa njia hiyo waweze kukabiliana nayo kwa tadibiri na umakini mkubwa na wasije wakafanya makosa katika mapambano hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Madola ya kibeberu yanataka kuwatoa Waislamu katika malengo yao makuu na kuwasahaulisha kazi ya kujiletea maendeleo yanayohitajika duniani kupitia kuzusha hitilafu katika safu za Waislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesema: Huko nyuma Wamagharibi walikuwa wanatekeleza njama zao hizo kupitia kuyakoloni mataifa ya Kiislamu na hivi sasa wanatumia mbinu ya kuzusha hitilafu kati ya Waislamu ili kufanikisha malengo yao ya kikoloni.
Amesisitiza kuwa: Tab'an Wamagharibi hata kwa kutumia kaulimbiu kama kuunga mkono na kutetea haki za binaadamu na kupigania demokrashia hawawezi kufuta doa jeusi la ukoloni lililowaganda.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa muhtasari wa hotuba yake hiyo kwa kusema: Kwa kuzingatia ramani ya njia ya adui, Waislamu wanapaswa kuwa na tabasuri na muono wa mbali, na kumjua vizuri adui yao na njama zake na watambue vyema pia kuwa, ramani ya njia ya Waislamu ni umoja, mshikamano, ushirikiano na mapenzi baina yao.
Mwanzoni mwa mkutano huo ambao ndani umehudhuria pia na wakuu wa Mihimili Mitatu Mikuu ya Dola (Serikali, Bunge na Mahakama) pamoja na Mkuu wa Halmashauri ya kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran ametoa hotuba fupi na sambamba na kutoa mkono wa baraka kwa kuwadia maadhimisho ya siku ya kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad SAW amesema kuwa: Mtume mtukufu wa Uislamu ni hazina ya elimu na mwelewa mkubwa wa dafina za siri za Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Amesema kuwa: Ujumbe mkuu wa Mtume Muhammad al Mustafa SAW ilikuwa ni kumwongoza mwanadamu na alipata tabu nyingi sana katika njia yake hiyo tukufu.
Ameongeza kuwa: Lengo la risala ya Mtume Mtukufu wa Uislamu ni kukamilisha matukufu ya kimaadili na kiakhlaki na ametumwa kwa wanadamu wote kama ambavyo upana wa risala yake unaihusu dunia nzima na ni kwa ajili ya ukamilifu wa binadamu wote.
Rais Ahmadinejad ameongeza kuwa: Mapinduzi adhimu ya Iran yaliyoongozwa na Imam Khomeini (quddisa sirruh) ni muendelezo wa njia ya saada na ufanisi ya Manabii wa Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa: Kusimamishwa kikamilifu tawhidi na uadilifu duniani ni ahadi ya haki ya Mwenyezi Mungu na ahadi hiyo itatimia kwa kudhihiri hazina ya mwisho ya Allah yaani Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake).