Maandamano makubwa ya Siku ya Kimataifa ya Quds yameanyika katika miji na mikoa yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Maandamano kama hayo ya kutetea Quds tukufu na kuunga mkono mapambano ya kupigania uhuru ya Wapalestina pia yanafanyika katika nchi mbalimbali duniani.
Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi mtukufu wa Ramadhani Waislamu na wapenda haki kote duniani hushiriki katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kupaza sauti zao dhidi ya Wazayuni maghasibu. Waandamanaji hao hutangaza mshikamano wao na Wapalestina ambao wanaendelea kukandamizwa na kufukuzwa katika ardhi za mababu zao, vitendo viovu ambavyo vinafanyika kwa uungaji mkono wa nchi za Magharibi zinazojidai kuwa mstari wa mbele katika kutetea uhuru na haki za binadamu.
Siku ya Kimataifa ya Quds inawakumbusha walimwengu misimamo imara ya hayati Imam Ruhullah Khomeini katika kupigania haki na uadilifu. Mwaka 1979 Imam Khomeini aliwataka Waislamu na wapenda haki kote duniani kuifanya Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds, kuiadhimisha siku hiyo kwa maandamano ya kutangaza hasira na chuki zao dhidi ya Maghasibu wa Israel, na vilevile kutangaza mshikamano wao na wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.
Katika kipindi chote cha miaka 46 iliyopita utawala ghasibu wa Israel umeendelea kuvamia ardhi za Wapalestina, kujenga vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi na kuchimba mashimo chini ya Msikiti wa Al Aqsa. Utawala huo pia unawazuia Waislamu kutekeleza ibada ya swala za jamaa na Ijumaa katika msikiti huo mtakatifu huku ukiendelea kuharibu utambulisho wa Kiislamu wa mji wa Baitul Muqaddas. Wazayuni wa Israel hawakutosheka na hayo bali wanafanya kila wawezalo kuharibu hata turathi za Kikristo zilizoko katika mji huo.
Ripoti zinasema kuwa sehemu kubwa ya misikiti ya kale ya Quds Mashariki imeharibiwa na kubomolewa na hata ile iliyobaki inakabiliwa na hatari ya kumobolewa na kujengwa vituo vya Kiyahudi mahala pake. Mbaya zaidi ni kuwa, Wazayuni wa Israel wanavunja misikiti ya ibada na kujenga vilabu na nyumba za anasa na starehe mahala pake.
Ripoti ya Wizara ya Wakfu ya Palestina inasema kuwa, zaidi ya misikiti 1200 imevunjwa tangu Wazayuni wavamie ardhi ya Palestina mwaka 1948.
Mji wa Quds ni kituo cha dini za Mwenyezi Mungu na kibla cha kwanza cha Waislamu na ulivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Wazayuni zaidi ya karne 4 sasa. Umoja wa Mataifa pia ulipasisha maazimio mawili yenye nambari 242 na 338 katika Baraza lake la Usalama ukisisitiza kuwa, mji wa Quds unakaliwa kwa mabavu. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitaka Israel iondowe jeshi lake katika mji huo, japo kuwa maazimio hayo mawili hayajatekelezwa hadi sasa kutokana na uungaji mkono mkubwa wa nchi za Magharibi hasa Marekani kwa utawala wa kikatili wa Israel.
Inatarajiwa kuwa maandamano makubwa ya leo katika maeneo mbalimbali duniani ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds yatazidisha moyo wa mapambano ya wananchi wa Palestina na kuongeza kasi ya kukombolewa Quds tukufu na ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu.
1266941