Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa hapa mjini Tehran amesema leo kuwa, Marekani na Waitifaki wake wa Ulaya na Mashariki ya Kati wakiishambulia kijeshi Syria watazidi kuchukiwa na Waislamu pamoja na wapenda haki kote duniani.
Hujjatul-Islam Kadhim Siddiqi amekumbusha kuwa, Marekani na Waitifaki wake wa Ulaya bado hawajajitoa kwenye kinamasi cha vita vya Iraq na Afghanistan na ametahadharisha kuwa, iwapo wataamua kuivamia Syria, watakuwa wanapigilia msumari wa mwisho kwenye majeneza yao. Amesema hatua zozote za kijeshi dhidi ya Syria zitalitikisa eneo zima la Mashariki na chuki dhidi ya Marekani itaongezeka maradufu katika ulimwengu wa Kiislamu. Akizungumzia kadhia ya Misri, hhatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa hapa mjini Tehran amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ingependa kuona mgogoro ulioko ukitatuliwa kwa njia ya amani. Hujjatul-Islam Kadhim Siddiqi amesema hali haiwezi kuwa nzuri iwapo jeshi la Misri litaendelea kuwakamata maafisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin na badala yake ametoa wito kwa serikali ya mpito kutafuta njia za amani za kutatua suitafahamu iliyoko. Amesema itakuwa pigo kubwa kwa Ulimwengu wa Kiislamu iwapo vita vya ndani vitaripuko huko Misri.
1280180