Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia imetangaza kuwa, kuna ushahidi wa kutosha unaothibitisha kuwa, video ya wahanga wa mauaji ya silaha za kemikali wanaodaiwa kuuliwa na jeshi la Syria, ni ya bandia.
Aidha Wizara hiyo imesisitiza kuwa wataalamu wa kimataifa wamewasilisha ushahidi wa kutosha katika duru ya 24 ya kikao cha kutetea haki za binaadamu iliyofanyika mjini Geneva, Uswisi ukionyesha kuwa video hiyo inayotumiwa na madola ya Magharibi ikiwemo Marekani kudai kwamba serikali ya Damascus ndiyo iliyohusika na shambulizi hilo huko katika mkoa wa Rif Dimashq, ni ya bandia. Katika kikao hicho, wajumbe wa kikao hicho walilaani vikali vitisho vya serikali ya Washington vya kutaka kuishambulia kijeshi Syria bila ya kibali cha Umoja wa Mataifa, na kusema kuwa, hatua hiyo inahesabiwa kuwa ni ukanyagaji ulio wazi wa sheria za kimataifa. Kwa upande mwingine Russia imetangaza kuwa hivi karibuni itawasilisha dondoo za mpango wake mpya wa kutatua kadhia ya silaha za kemikali huko nchini Syria. Leo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia Sergey Lavrov amesema kuwa, Moscow kwa kushirikiana na serikali ya Damascus, itawasilisha mpango huo ulio wazi wa kutatua kadhia hiyo na kuzikabidhi pande husika ikiwemo Marekani. Aidha Lavrov amesisitiza juu ya udharura wa kukamilishwa uchunguzi wa watafiti wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria. Amesema kuwa, wale wote waliohusika na utumiwaji wa silaha hizo, lazima waadhibiwe. Hii ni katika hali ambayo serikali ya Syria imekaribisha pendekezo la Moscow la kuziweka silaha zake za kemikali chini ya uangalizi ya Umoja wa Mataifa. Aidha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu nayo imekaribisha mpango huo wa Russia kuhusiana na kadhia ya silaha za kemikali za Syria. Hii ni katika hali ambayo Katibu Mkuu wa chama cha Demokrasia nchini Lebanon amesema kuwa, hatua ya kusitishwa mashambulizi ya Marekani nchini Syria, imetokana na uwezo wa harakati za muqawama katika eneo hili. Walid Barakat amesisistiza kuwa, lengo la Marekani la kutaka kuishambulia kijeshi nchi hiyo ya Kiarabu, ni kujaribu kusambaratisha muqawama katika eneo la Mashariki ya Kati na kwamba, uwezo mkubwa wa muqawama unaoanzia nchini Iran hadi Lebanon, umeifanya serikali ya Washington, kuogopa kuivamia kijeshi Syria.
1286393