IQNA

Maandamano ya kulaani kuvunjiwa heshima Mtume SAW

6:40 - January 18, 2015
Habari ID: 2720426
Waislamu wa kila pembe duniani wameendelea kulaani vikali kitendo cha jarida linalochapishwa Ufaransa la Charlie Hebdo cha kuchapisha tena picha za vikatuni vya kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW.

Miji mbalimbali hapa nchini Iran na katika nchi za Pakistan, Azarbaijan, Jordan, Kuwait, Syria, Yemen, Lebanon, Uturuki, Palestina, Tunisia, Sudan, Mauritania, Mali, Misri, Niger na Algeria imeshuhudia maandamano ya kupinga na kulaani kuchapishwa katuni hizo katika jarida hilo.

Huko nchini Niger watu wasiopungua wanne akiwemo askari polisi na raia watatu wameuawa na wengine 45 wamejeruhiwa wakati Waislamu wenye hasira waliposhambulia kituo cha utamaduni cha Ufaransa katika mji wa pili kwa ukubwa wa Zinder.

Nchini Jordan waandamanaji wenye hasira wamesisitiza kuendelea na maandamano hadi ubalozi wa Ufaransa nchini humo uwaombe radhi Waislamu. Waandamanaji katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum wametaka balozi wa Ufaransa aondoke nchini humo. Mbali na radiamali ya wananchi wa mataifa ya Kiislamu viongozi wa nchi mbalimbali za Kiislamu pia wametoa radiamali za kulaani kitendo cha jarida la Charlie Hebdo cha kuchapisha tena picha za katuni za kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW. Viongozi hao wakiwemo marais wa Pakistan, Afghanistan na Uturuki wamelaani kitendo hicho na kulitaka jarida la Charlie Hebdo liombe radhi. Wakati huohuo gazeti la al Watan linalochapishwa nchini Saudi Arabia limeandika kuwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) inachunguza uwezekano wa kufungua mashtaka dhidi ya jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo. Akizungumza katika mahojiano na gazeti hilo Katibu Mkuu wa OIC Iyad Madani amesema jumuiya hiyo inachunguza sheria zinazohusiana na uhuru wa maoni pamoja na kanuni zake nchini Ufaransa na Ulaya ili kuandaa utangulizi wa kuchukua hatua za kulifatilia gazeti hilo kupitia vyombo vya sheria. Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Septemba mwaka 2012, jarida la Charlie Hebdo lilichapisha picha za katuni za kumtusi na kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW na kuamsha wimbi kubwa la ghadhabu na malalamiko ya Waislamu duniani…/mh

2718150

captcha