IQNA

Rais wa Iran alaani kuvunjiwa heshima Mtume SAW

0:27 - January 22, 2015
Habari ID: 2743220
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya udharura wa kujiepusha na ugaidi, misimamo mikali na utumiaji mabavu kwa kisingizio cha kulinda dini.

Rais Rouhani ameashiria matukio yaliyotokea hivi karibuni Paris nchini Ufaransa na kusema Iran inapinga ugaidi, utumiaji mabavu na misimamo mikali kwa kisingizio cha kulinda dini na wakati huo huo inalaani vitendo vya dharau, kebehi na kuchochea hisia za wafuasi wa dini mbalimbali kwa kisingizio cha kulinda uhuru. Amesema vitendo vya kuua watu na kufanya ugaidi haviwezi kunasibishwa na Waislamu au na dini ya Uislamu na kwamba wanaofanya hivyo wanausaliti Uislamu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kitendo kingine kiovu kilichofanyika Ufaransa ni kuvunjiwa heshima itikadi na matukufu ya Waislamu bilioni moja na nusu na kwamba vitendo hivyo vinavyofanyika kwa kisingizio cha kutetea uhuru vinachochea hisia za Waislamu. Akizungumza mjini Tehran Jumanne usiku, Rais Rouhani aliongeza kuwa  Mtume Muhammad SAW si wa Waislamu pekee bali pia anaenziwa na kupewa heshima na wasomi, wanafikra na shakhsia wakubwa kote duniani. Amesema anasikitika kuona vitendo viovu kama hivyo vinafanyika katika nchi inayodai kutetea uhuru na kuongeza kuwa, maafa makubwa zaidi ni kuwa katika dunia ya leo vitendo vya kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini na kuchochea hisia za watu wengine vinatambuliwa kuwa ni uhuru wa kusema na kujieleza.

Rais Rouhani amesisitiza kuwa, vitendo hivyo vinazidisha harakati zenye misimamo mikali na kuonesha kuwa kuna njama za nyuma ya pazia ambazo hazitaki kuona ulimwengu wa Kiislamu ukiwa na uhusiano mwema na maeneo mengine ya dunia.

2738781

captcha