IQNA

Serikali ya Italia yapinga sheria dhidi ya Msikiti

18:57 - March 14, 2015
Habari ID: 2983062
Serikali kuu ya Italia imekwenda kwenye mahakama ya Katiba kupinga sheria mpya iliyopitishwa na serikali ya ndani ya jimbo la Lombardy la kaskazini mwa nchi hiyo.

Serikali ya Waziri Mkuu, Matteo Renzi imeamua kuchukua hatua hiyo baada ya kushadidi ukosoaji wa Waislamu na wapigania haki nchini Italia kwa sheria hiyo ya jimbo la Lombardy. Serikali ya jimbo la Lombardy mwanzoni mwa mwaka huu ilipitisha sheria mpya inayolenga kudhibiti ujenzi wa majengo mapya ya ibada kwa dini za walio wachache jimboni humo. Sheria hiyo ikitekelezwa, Waislamu watatakiwa kutimiza masharti magumu mno kabla ya kuruhusiwa kujenga msikiti mpya kwenye eneo hilo. Wachambuzi wengi wanasema ingawa sheria hiyo haikutaja misikiti, ni wazi kuwa masharti yasiyotekelezeka kwenye sheria hiyo yanalenga kuwabana Waislamu wasiopungua milioni moja nchini Italia na ambao dini yao haitambuliwi rasmi kisheria katika nchi hiyo ya Ulaya yenye idadi kubwa ya Wakrito wa Kikatoliki. Inatarajiwa kuwa, mahakama ya katiba ya Italia itabatilisha sheria hiyo kwani wataalamu wa sheria za Italia wanasema sheria ya jimbo la Lombardy dhidi ya nyumba za ibada inakiuka haki za msingi za wananchi zinazolindwa na katiba ya nchi.../mh

2980933

captcha