Akizungumza na IQNA pembezoni mwa maonyesho hayo, Profesa Chiara Sebastiani wa Chuo Kikuu cha Bologna alibainisha kuwa Waislamu kote ulimwenguni wanakabiliana na changamoto za kipekee kulingana na mazingira yao ya ndani. Amesema kuwa majukwaa kama haya yanatoa fursa kwao kuungana na kusaidiana.
"Ni muhimu sana kwa jamii za Kiislamu katika nchi mbalimbali kushirikiana uzoefu wao na pia mahitaji maalum ya jamii zao," alisema. "Waislamu katika kila nchi wana mahitaji na changamoto tofauti."
Profesa huyo alieleza kuhusu hali ya Waislamu nchini Italia, ambako jamii ya Kiislamu ni ndogo na ya hivi karibuni. "Huko Italia, sisi ni jamii ndogo na ya hivi karibuni. Kwa hivyo, ni muhimu sana kuweza kuwasiliana na nchi za Kiislamu na kujifunza kutoka kwa uzoefu wao," alieleza.
Pia amesisitiza umuhimu wa maonyesho haya kama jukwaa la kukuza mazungumzo, kuelewana kwa pande zote, na kushirikiana miongoni mwa Waislamu ulimwenguni.
"Nadhani moja ya majukumu muhimu ya maonyesho kama haya ni hasa hili: fursa ya kufahamiana, kubadilishana uzoefu, na kusaidiana kwa pande zote," alisema.
Maonyesho hayo yalifunguliwa Jumatano na yataendelea hadi Machi 16, yakifanyika kila siku kuanzia saa 10 jioni hadi saa 5 usiku (saa za Tehran) katika Mosalla Imam Khomeini jijini Tehran.
Maonyesho ya mwaka huu yanajumuisha programu mbalimbali, ikiwemo vikao maalum, warsha za kielimu, mikusanyiko ya Qur'ani, na shughuli maalum kwa watoto na vijana.
Toleo la 32 la maonyesho hayo linachukua takriban mita za mraba 20,000, likiwa na sehemu 37 za maudhui na uendeshaji.
Maonyesho haya hufanyika kila mwaka katika mwezi mtukufu wa Ramadhani chini ya uratibu wa Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu ya Iran.
Lengo lake ni kueneza fikra za Qur'ani na kuendeleza shughuli za Qur'ani nchini Iran na duniani. Pia linaonyesha mafanikio ya hivi karibuni ya Qur'ani nchini Iran pamoja na aina mbalimbali za bidhaa zinazolenga kuhimiza usomaji na uelewa wa Qura'ani.
3492305