Kwa mujibu wa mashuhuda, mripuko huo wa bomu ulitokea jana katika soko la nyama ambalo lilikuwa limefurika watu katika mji huo ambao ni makao makuu ya jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Baadhi ya watu wanasema kuwa, bomu hilo lililokuwa limetegwa chini ya meza ya muuza nyama mmoja sokoni hapo, huku wengine wakisema kuwa, mlipuko huo ulitokana na mtu aliyekuwa amevalia bomu, kujiripua katikati ya watu. Duru za afya mjini hapo, zinasema kuwa idadi ya wahanga wa shambulio hilo lililotokea majira ya saa saba ya mchana kwa majira ya nchi hiyo, imeongezeka na kufikia 60, na kwamba kuna uwezekano idadi hiyo ikaongezeka kutokana na kwamba watu wengi walijeruhiwa baadhi wakiwa mahututi. Ingawa hadi sasa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram bado halijatangaza kuhusika na hujuma hiyo, lakini kidole cha lawama kimeelekezwa kwa kundi hilo ambalo limekuwa likitekeleza jinai kama hizo. Watu 26 waliuawa na wengine 28 kujeruhiwa Jumamosi iliyopita wakati walipokuwa wakisali katika msikiti mmoja wa mji huo, baada ya mwanachama wa kundi la Boko Haram kujiripua msikitini hapo.
Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Zaidi ya watu elfu 13 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009. Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila nchini humo.../mh