IQNA

Vijana wa Sudan wazindua 'Mpango wa Rehema' Mwezi wa Ramadhani

16:55 - June 25, 2015
Habari ID: 3318508
Muungano wa Vijana wa Sudan wamezindua 'Mpango wa Rehema' chini ya anwani ya: "Ramadhani Inatuleta Pamoja".

Mpango huo ulizinduliwa hivi karibuni na unajumuisha msafara wa Daawa, zahanati za muda, mashindano ya Ramadhani, futari kwa wapita njia, kukarabati misikiti, kuandaa mashindano ya michezo na hatimaye kutoa zawadi za nguo kwa mnasaba wa Siku Kuu ya Idul Fitr kwa familia za wasiojiweza katika nchi hiyo ya Afrika.
Akizungumza na waandishi habari, Waziri wa Usalama wa Jamii Sudan Ibrahim Adam Ibrahim amepongeza mpango huo wa vijana wa Sudan na kusema jamii inahitaji ubunifu kama huo unaowalenga watu wasiojiweza katika jamii. Aidha ametoa wito kwa Wasudani kuendeleza mafundisho ya Kiislamu ya kuwasaidia wasiojiweza. Mwenyekiti wa Muungano wa Vijana wa Sudan Dkt. Shogar Bashar amesema mpango huo utajumuisha majimbo yote ya nchi hiyo na kwamba tayari kuna misafara tayari imeshatumwa katika maeneo mbali mbali. Amesema muungano huo umeshakarabati misikiti zaidi ya 3,000 na kutayarisha vifurushi 80,000 vya chakula kwa ajili ya familia masikini katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.../mh

3317715

captcha