IQNA

Sera za Iran kuhusu Ukombozi wa Palestina

12:07 - July 09, 2015
Habari ID: 3325960
Moja ya mafanikio makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu ni kuifanya kadhia ya Palestina kuwa kadhia nambari moja katika ulimwengu wa Kiislamu.

Baada ya kukaliwa kwa mabavu Palestina na Wazayuni, serikali za Kiarabu kidhahiri zilitangaza kuzingatia kadhia ya Palestina na ni kwa msingi huo ndio Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC ikaundwa huku lengo lake kuu likiwa ni kuikomboa Quds Tukufu. Baadhi ya serikali za Kiarabu zilifanya kosa la kistratijia kwa kuigeuza kadhia ya Palestina kuwa  ya Kiarabu. Nchi za Kiarabu zilifanya kosa hilo baada ya vita vitatu na Wazayuni ambapo zilipoteza ardhi zao na hivyo kutengwa katika Umma wa Kiislamu. Anwar Sadat Rais wa Misri aliyeuawa, alikuwa kiongozi wa kwanza wa nchi za Kiarabu kutia saini mkataba na Wazayuni. Mkataba huo wa mwaka 1978 wa Camp David ulitoa pigo kubwa sana kwa harakati za ukombozi wa Palestina.
Imam Khomeini (MA) atangaza Siku ya Kimataifa ya Quds
Lakini pamoja na hayo, katika upande wa pili wa ulimwengu wa Kiislamu, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi mwaka 1979 na punde baada ya hapo, Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akaitangaza Ijumaa ya Mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Quds na kwa msingi huo kuifanya kadhia ya ukombozi wa Palestina kuwa kadhia yenye kupewa umuhimu mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Imam Khomeini aliamini kuwa, utawala wa Kizayuni ni donda la saratani na pandikizi na lenye kutoka nje ya mipaka ya ubinadamu. Aliamini kuwa utawala bandia wa Israel ulibuniwa na Mayahudi na madola makubwa yaliyopata ushindi katika vita vikuu vya pili vya dunia. Madola hayo yaliwakusanya Mayahudi kutoka kila kona ya dunia na kuwaingiza Palestina jambo ambalo lilipelekea idadi kubwa ya Wapaletina kuwa wakimbizi.  Aliamini kuwa mpango huu wa kimataifa si tu kuwa haukuwa wa sadfa au kama wanavyosema kufidia dhulma na mauaji waliotenda Manazi dhidi ya Mayahudi, bali ilikuwa ni njama iliyoratibiwa kwa njia maalumu dhidi ya Waislamu. Ni kwa msingi huu ndio Imam Khomeini MA akaamini kuwa Israel ni donda la saratani lililopandikwza miongoni mwa nchi za Kiislamu na kwamba linapaswa kuondolewa. Imam Khomeini MA alibainisha fremu ya kinadharia na kivitendo ya sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu Palestina katika kipindi cha miaka 10 alipokuwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei aendeleza sera za Imam kuhusu Palestina
Naye Ayatullah Khamenei, aliyechukua nafasi ya Imam Khomeini MA, pia ametegemea msingi huo huo katika kuongoza sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu uvamizi wa utawala wa Kizayuni. Katika minasaba mbali mbali na mikutano na wananchi, na viongozi wa mapambanpo walio mstari wa mbele wa mapambano ya Kiislamu dhidi ya utawala wa Kizayuni huko Lebanon na Palestina, amebainisha utambulisho wa utawala wa Kizayuni na udharura wa kupambana na utawala huo bandia. Hujuma za utawala wa Kizayuni huko Lebanon na uvamizi wa mara kadhaa wa utawala huo huko Ghaza sambamba na mashambulizi ya mara kadhaa dhidi ya Wapalestina wanaoishi Ukingo wa Magharibi  na Quds Tukufu ni mambo ambayo yamepelekea wote kudiriki na kufahamu msimamo na mtazamo wa Imam Khomeini MA na Ayatullah Khamenei kuhusu utambulisho wa utawala wa Kizayuni.  Hivi karibuni kulichapishwa kitabu chini ya anwani:  "Palestina Kwa Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu". Kitabu hiki cha kurasa 414 kinabainisha mitazamo ya Hadhrat Ayatullah Khamenei kuhusu Palestina katika fremu ya hotuba na risala zake.
Kuhusu maudhui ya Palestina na kubakisha hai mkakati wa ukombozi wa Palestina na umuhimu wa suala hilo kwa kila Mwislamu, Ayatullah Khamenei anaamini kuwa: "Suala muhimu zaidi leo ni suala la Palestina. Katika nusu karne iliyopita suala hilo limekuwa suala muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu na pengine suala muhimu zaidi kwa jamii ya mwanadamu.  Hapa tunazungumzia masaibu, kufanywa wakimbizi na kudhulumiwa taifa. Tunazungumzia kughusibiwa nchi. Tunazungumzia kupandikizwa donda la saratani katika kitovu cha nchi za Kiislamu na katika eneo lenye kuunganisha magharibi na mashariki mwa ulimwengu wa Kiislamu. Hapa tunazungumzia dhulma endelevu ambayo imevikumba vizazi viwili vya taifa la Waislamu wa Palestina mfululizo. Leo kuna mwamko uliojaa damu wa watu wa Palestina ambao wanakabliwa na hatari ya wazi ya Wazayuni maghasibu huku jamii ya kimatiafa ikinyamazia kimya jinai hizo. Jambo hili linatukumbusha kuwa adui anapanga njama kali sana na hivyo Waislamu kote duniani wanapaswa kulipatia suala hili uzito mkubwa.
Njama za Uingereza kuhusu Palestina
Hizi ndizo habari za zama zetu hizi…"Kati ya nukta muhimu kuhusu kadhia ya Palestina ni namna ulivyoundwa utawala wa Kizayuni na kufukuzwa Wapalestina kutoka ardhi zao za jadi. Leo kumeibuliwa shubha kubwa sana kuwa Wapalestina waliwauzia Mayahudi ardhi zao na kwa hivyo wanaulizwa ni kwa nini wanataka kuchukua tena ardhi zao walizouza? Ayatullah Khamenei katika kujibu swali hili anasema hivi: "Awali Waingereza walipoingia Palestina hawakusema 'sisi tunawaingiza wahajiri hapa Palestina.' Watu wa Palestina walistaajabu hawa ni kina nani wanaokuja!? Waingerea waliwahadaa na kusema: "Tunawaleta wataalamu"!.  Haya tunayoyasema ni mambo yenye ushahidi na yalifichuliwa katika nyaraka za Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza. Baadhi ya wizara za mambo ya nje katika maeneo mbali mbali duniani husambaza nyaraka za siri za kale na kuziweka wazi kwa wote. Nyaraka ninazoashiria sasa, zimetangazwa wazi baada ya miaka sitini. Katika nyaraka hizi, afisa wa Uingereza aliyekuwa anafanya kazi Palestina aliandika hivi katika ripoti yake: "Sisi tumewaambia watu wa Palestina kuwa watu wanaokuja Palestina ni wataalamu na wahandisi na wanakuja kuijenga nchi yenu! Na wakishaijenga nchi yenu wataondoka.' Afisa huyo wa Uingereza katika barua yake moja aliandika hivi: "Lakini sisi tuliwadanganya hawa watu! Mayahudi wasio wataalamu na wasio na taaluma wamekusanywa kutoka kote duniani na kuletwa Palestina na kupewa ardhi pamoja na suhula zote hapo. Hii ni kwa sababu (hao Mayahudi) walikusudia tokea mwanzo kuwatimua wakaazi asili wa Palestina. Awali waliingia kwa ujanja na udanganyifu na punde baada ya kujiimarisha walianza kushambulia."
Mtazamo wa Hadhrat Ayatullah Khamenei kuhusu masuala ya Palestina ni mtazamo wa kina.  Kwa kutegemea ujuzi kamili wa utambulisho wa utawala wa Kizayuni, yeye hutoa  miongozo,  risala  na hotuba mbali mbali katika mikutano na viongozi wa harakati za Mapambano ya Kiislamu Lebanon na Palestina na kuwabainishia Waislamu wazi kuhusu vitisho  mbali mbali vya utawala wa Kizayuni. Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hatazami maudhui ya Palestina kama maudhui ya Wapalestina tu bali ameitaja kadhia ya Palestina kuwa ni kadhia ya ulimwengu mzima wa Kiislamu. Aidha amekutaja kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na pahala pake kuundwa utawala bandia na wa kibaguzi wa Israel kuwa ni dhulma kubwa dhidi ya ubinadamu. Kuhusu hili, Ayatullah Khamenei anasema: "Dhulma inayotendewa Wapalestina haijawahi kutendewa taifa jingine lolote." Kutetea malengo ya ukombozi wa Palestina na kupinga aina yoyote ya maelewano na Wazayuni ni moja ya fikra za kimsingi za Ayatullah Khamenei. Amekutaja kutetea Wapalestina kuwa ni  wajibu kwa kila Mwislamu na kwamba utawala wowote usio wa Palestina ni utawala ghasibu. Ayatullah Khamenei ametangaza wazi kuwa: "Sisi tunaitambua kuwa wajibu jihadi dhidi ya Wazayuni."
Uungaji mkono wa Iran kwa Palestina haushii masuala ya kisiasa
Uungaji mkono wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa harakati ya ukombozi wa Palestina haushii tu katika uungaji mkono wa kisiasa. Tokea mwanzo wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijasita kuwapa wanamapambano wa Palestina misaada mbali mbali iwe ni ya kimaanawi, kisiasa na kifedha. Kuhusu nukta hiyo Ayatullah Khamenei anasema: "Kila sehemu inapotetewa Palestina, sisi tuko hapo."  Hafla adhimu zaidi duniani ya Siku ya Kimataifa ya Quds hufanyika katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani nchini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Siku ya Kimatiafa ya Quds hapa Iran sasa imegeuka kuwa takribani siku ya kitaifa. Sala ya Ijumaa katika Siku ya Kimataifa ya Quds mjini Tehran na mamia ya miji mingine kote Iran huwa tafauti na sala zote za Ijumaa katika mwaka.  Viongozi wa harakati za Kiislamu za ukombozi wa Palestina kwa mara kadhaa wameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uungaji mkono wake wa dhati na wenye faida kwa harakati za ukombozi wa Palestina hasa mapambano ya Wapalestina katika  Ukanda wa Ghaza. Ismail Haniya Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Kiislamu ya Ukombozi wa Palestina Hamas, alibainisha msimamo wake wa hivi karibuni kuhusu nafasi ya Imam Khomeini MA katika kuhuisha mapambano na kuunga mkono ukombozi wa Quds, alipofanya mazungumzo ya simu na Ali Akbar Salehi Makamu wa Rais wa Iran mwanzoni mwa mwezi Juni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuaga dunia Imam Khomeini. Ismail Haniya aliashiria namna Imam Khomeini MA alivyohuisha utamaduni wa kutetea Quds na Palestina. Aidha Ismail Haniya alitoa shukrani zake za dhati kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi na rais wa Iran kwa misimamo yao imara na yenye taathira nzuri kuhusu Palestina na uungaji mkono kwa waliodhulumiwa. Kuhusiana na kadhia ya Palestina, Hadhrat Ayatullah Khamenei pia amewasilisha njia muafaka ya kidemokrasia ya utatuzi wa kadhia hiyo kwa kusema: "Kuhusu kadhia ya Mashariki ya Kati kuna njia moja tu iliyopo nayo ni kuvunjiliwa mbali serikali ya Kizayuni. Wakimbizi wote wa Palestina wanapaswa kurejea katika nchi yao. Watu hawa takribani milioni nane ndio wamiliki na wananchi halisi wa Palestina. Taba'an aghalabu ya watu wa Palestina ni Waislamu na wachache miongoni mwao ni Wapalestina Mayahudi na Wakristo. Wapalestina asili waunde serikali. Serikali hiyo iamuwe iwapo wale wote waliohamia ndani ya Palestina kutoa nchi zingine duniani wabakie hapo na iwapo wanabakia watabakia kwa masharti gani au waondoke."
Tukilinganisha fikra za Ayatullah Khamenei na fikra za Imam Khomeini MA amrehemu tunafikia natija kuwa, shakhsia hawa wawili wanaamini kuwa Israel ni msururu wa ukoloni na uistikbari wa kimataifa na njia ya kutatua kadhia hiyo ni ya kimsingi na ifuatwe hadi katika mzizi wake. Kwa mtazamo wa Ayatullah Khamenei, hakuna faida kufanya mazungumzo yoyote yale na utawala wa Kizayuni na kwamba Waislamu wanapaswa kutumia uwezo wao wote kuikomboa Quds. Uzoefu wa miaka 60 iliyopita katika eneo la Mashariki ya Kati hasa mazungumzo ya muda mrefu na yasiyo na natija ya miaka 20 ya Mashariki ya Kati chini ya anwani ya 'mazungumzo ya amani' ni jambo linaloidhinisha mtazamo huo.../mh

3325693

captcha