IQNA

Madrasah ya karne moja ya kufundisha Qur'ani karabatiwa nchini Uganda

17:06 - August 26, 2015
Habari ID: 3353009
Madrassah ya kufundishia Qur’an yenye umri wa zaidi ya karne nchini Uganda, itazamiwa kukarabatiwa upya hivi karibuni ili kuendelea kutumika kwa ajili ya kutoa mafunzo sahihi ya dini ya Kiislamu.

Hayo yamesemwa na mkurugenzi mtendaji wa televisheni ya Kiislamu ya nchini humo SALAM TV, al-Haji Karim Kalisa, ambaye amesema kuwa tayari kampeni za kukusanywa fedha za ukarabati wa shule hiyo ya Lukalu zimeanza. Kalisa ameongeza kuwa, shule hiyo ya Lukalu itakuwa kitovu cha kutoa mafundisho asili ya dini ya Kiislamu nchini Uganda na kwamba hadi sasa tayari zimekusanywa fedha zaidi ya Dola laki moja na elfu 41 za Kimarekani kwa ajili ya shughuli hiyo. Amefafanua kuwa, ukarabati wa kituo hicho cha Qur’an utaanza hivi karibuni. Aidha al-Haji Karim Kalisa amesema kuwa, redio na asasi kadhaa ambazo zimefanikisha kuasisiwa kanali ya televisheni ya Kiislamu ya SALAM TV, kupitia fremu ya kutoa elimu kwa Waislamu, zimekuwa zikifanya juhudi kubwa zenye lengo la kuiarifisha sura halisi ya dini hii ya mbinguni suala ambalo linaonekana kuwa na mafanikio. Mkurugenzi mtendaji wa televisheni hiyo ya Kiislamu ameongeza kuwa, tangu kanali hiyo ilipoanza kurusha matangazo yake, imefanikiwa kuwavutia watu wa jamii tofauti, Waislamu na wasiokuwa Waislamu pia. Uislamu uliingia Uganda mnamo mwaka 1884 Miladia, na ni kuanzia hapo ndipo kituo hicho cha Qur’ani kilipojengwa na vilevile shule nyingine za Kiislamu.

3350917

captcha