IQNA

Kijana wa Kipalestina Akuta Msahafu Uliosalimika Chini ya Magofu ya Nyumba Yake Gaza +Video

23:08 - October 15, 2025
Habari ID: 3481371
IQNA – Kijana mmoja wa Kipalestina amegundua nakala ya Msahafu ikiwa salama kabisa chini ya magofu ya nyumba yake iliyoharibiwa kaskazini mwa Gaza, akieleza hisia za kina na shukrani baada ya miezi ya mashambulizi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Al-Watan, Khaled Sultan, kijana wa Kipalestina, alirudi kwenye magofu ya nyumba ya familia yake iliyobomolewa na majeshi ya Israel na  alipokuwa akichambua kifusi, macho yake yalijaa hisia mseto za furaha, huzuni na hofu, moyo wake ukidunda kwa nguvu alipokaribia mahali palipokuwa chemchemi ya kumbukumbu na ndoto.

Sultan alieleza jinsi alivyotembea katikati ya magofu ya mahali alipoishi utotoni, akikumbuka nyakati alipokuwa pamoja na familia yake. Kati ya uharibifu huo wote, ghafla aliona kile alichokiita ishara ya kimungu nayo ilikuwa ni nakala ya Qurani Tukufu iliyosalimika bila kuguswa wakati wa kuharibiwa nyumba.  

Aliisoma aya iliyokuwa wazi katika ukurasa huo: "Basi furahini kwa biashara mliyofanya naye; na hiyo ndiyo mafanikio makubwa." (Surat At-Tawbah, aya ya 111)

Sultan alisema aya hiyo ilihisi kama “ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu,” ikithibitisha kuwa kujitolea kwa Wapalestina — nyumba zao na wapendwa wao — hakukuwa bure, bali ni sehemu ya njia kuelekea “ushindi mkubwa.”

Akiwa amesimama katikati ya magofu, alinyanyua mikono yake juu kwa shukrani na kusema: "Nyumba yetu imeharibiwa, lakini namshukuru Mwenyezi Mungu. Siwezi kuamini kuwa nimerudi nyumbani. Nyumba yetu kaskazini mwa Gaza imegeuka kuwa kifusi, lakini nina furaha kuwa hapa. Kwangu, hii ni ya thamani zaidi kuliko majumba yote ya kifalme duniani."

Zaidi ya Wapalestina 67,000 waliuawa katika kipindi cha miaka miwili ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yaliyoanza tarehe 7 Oktoba, 2023. Mashambulizi hayo makali ya Israel yaliyotekelezwa kwa msaada wa Marekani, yamebomoa au kuharibu majengo mengi katika eneo la Gaza lililozingirwa. Usitishaji wa mapigano ulianza Gaza siku ya Ijumaa, kufuatia tangazo la awali kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump.

3495018

Habari zinazohusiana
captcha