IQNA

“Alisimulia Upya Tukio la Karbala”: Mwanazuoni Azungumzia Uongozi wa Bibi Zaynab (SA) Katika Upashaji Habari

16:10 - October 27, 2025
Habari ID: 3481426
IQNA – Bibi Zaynab (SA) “ndiye aliyekuwa wa kwanza kukabiliana na upotoshaji kwa kutumia mbinu zinazofanana na zile za vyombo vya habari vya leo—kufichua, kutafsiri upya, na kusimulia tena ukweli,” amesema mtafiti kutoka Iran.

Hujjatul-Islam Meisam Ghasemi, mtafiti na mhadhiri mwenye shahada ya uzamivu katika masomo ya Kiislamu, alikuwa akizungumza kuhusu nafasi ya Bibi Zaynab (SA) katika harakati ya Imam Hussein (AS).

Katika mahojiano na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA), alisisitiza kuwa matendo ya Bibi Zaynab (SA) yanapaswa kueleweka ndani ya muktadha mpana wa uongozi wa wanawake katika historia ya Kishia, badala ya kuchukuliwa kama matukio ya pekee.

“Katika muktadha huu, wanawake katika historia ya Kishia hawakutimiza tu majukumu ya kielimu au kihisia, bali walicheza nafasi za msingi na za kudumu katika nyanja za kijamii, kisiasa, kitamaduni na hata za vyombo vya habari,” alisema.

Amebaini kuwa msiba wa Karbala na matokeo yake ulidhihirisha jinsi Bibi Zaynab (SA) na wanawake wengine walivyovuka mipaka ya majukumu ya kusaidia tu.

Baada ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS) na masahaba wake katika vita vya Karbala mwaka mwaka 61 Hijria au 680 Miladia, Bibi Zaynab (SA) alijitokeza kama kiongozi mkuu. Kwa mujibu wa masimulizi ya kihistoria, alisimamia ustawi wa wanawake na watoto katika kambi ya Karbala, na baada ya mauaji hayo, alikabiliana na watekaji katika mahakama za Kufa na Damaascus kwa hotuba zenye nguvu zilizofichua dhulma na kusaidia kulinda ujumbe wa Imam Hussein (AS).

Harakati ya Imam Hussein (AS) inachukuliwa kama tukio la kihistoria linalofafanua misingi ya Uislamu wa Kishia. Ilibeba alama ya kupinga dhulma na kuthibitisha misingi ya haki na kujitolea. Nafasi ya Bibi Zaynab (SA) baada ya vita, ambayo mara nyingi hufafanuliwa kama “mchukuzi wa ujumbe wa Karbala”, ilihakikisha kuwa simulizi la tukio hilo liliendelezwa na halikufutwa wala kusahaulika.

Hujjatul-Islam Ghasemi alieleza kuwa uongozi wa Bibi Zaynab (SA) ulikuwa na vipengele viwili vikuu: “nafasi ya kuunganisha” ambapo aliunda uhusiano kati ya walionusurika Karbala, Ahlul Bayt wa Imam Hussein (AS), na jamii pana ya Waislamu; na “nafasi ya kudumisha” ambapo alitumia ufasaha wa hotuba, akili ya kihisia, na uwazi wa kimaadili kulinda ujumbe dhidi ya upotoshaji.

“Kilichofanywa na Zaynab hakikuwa tu kufichua historia; bali kilikuwa ni kujenga upya simulizi la kimungu lililochota ukweli kutoka katika kiini cha msiba na kuamsha dhamiri ya historia,” alihitimisha.

Ikumbukwe kuwa, katika siku kama ya leo miaka 1442 iliyopita alizaliwa Bibi Zaynab (SA) binti mtukufu wa Imam Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatimatu Zahraa (AS).

Bibi Zaynab alikuwa mashuhuri miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo.

Katika tukio la Karbala, Bibi Zaynab (SA) alisimama kidete na kukabiliana na dhulma za watawala dhalimu na ujahili watu wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (AS). Bibi Zaynab alipelekwa Sham pamoja na mateka wengine wa Nyumba Tukufu ya Mtume (SAW) baada ya mapambano ya Imam Hussein (AS) huko Karbala. Hotuba za Bibi Zainab mbele ya majlisi ya Ibn Ziyad, mtawala wa Kufa na katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko Sham zilikuwa na taathira kubwa katika kufichua dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya na kuonesha jinsi Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume walivyodhulumiwa.   

3495169

Kishikizo: bibi Zaynab karbala
captcha